Ali Bagheri Kani ameeleza hayo jana katika hotuba yake mbele ya mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani na kuongeza kuwa, takriban watu 20 wanauawa au kujeruhiwa ndani ya kila saa moja huko Gaza, huku zaidi ya asilmia 80 ya maeneo ya makazi na miundombinu yote, ikijumuisha hospitali, misikiti, makanisa, vituo vya elimu, na maeneo ya kihistoria, ikiharibiwa.
Kani ameashiria jinai za Israel huko Gaza katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, ambazo zimesababisha mauaji ya watu wasio na hatia, akthari yao wakiwa ni wanawake na watoto.
Amefafanua kwa kusema, “Katika muda wa siku 285 zilizopita, utawala unaoikalia kwa mabavu Palestina umekuwa ukifanya jinai kubwa dhidi ya binadamu huko Gaza. Utawala huu, kupitia kampeni ya ukatili na ugaidi, unaendelea kuwaua watu wasio na hatia, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.”
Kadhalika Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameishutumu Marekani kwa vita vya mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza umuhimu wa kushirikiana pande kadhaa ili kurejesha amani na utulivu duniani.
Mkutano huo wa Baraza la Usalama la UN umefanyika katika hali ambayo, idadi ya mashahidi wa Kipalestina waliouawa tangu kuanza hujuma za kinyama za jeshi la utawala wa Kizayuni huko Gaza (Oktoba 7, 2023) imekaribia watu 39,000.
342/