30 Julai 2024 - 19:33
Pezeshkian amekula kiapo mbele ya Bunge kama rais wa 9 wa Iran

Daktari Masoud Pezeshkian leo alasiri amekula kiapo kama rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge), na viongozi kutoka nchi zaidi ya 88 waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwake.

Rais Pezeshkian amekula kiapo hicho kwa kitabu kitakatifu cha Qur'ani katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu na kuhudhuriwa na Mkuu wa Idara ya Mahakama, Gholamhossein Mohseni-Ejei, wabunge, maafisa wa ngazi za juu wa dola na wageni waalikwa kutoka maeneo yote ya dunia.

Pezeshkian aliapa kuilinda dini rasmi ya nchi, yaani Uislamu,  Jamhuri ya Kiislamu na Katiba. Aliendelea kusema kuwa: "Nitajitolea kwa uwezo na sifa zangu zote ili kutimiza majukumu niliyokabidhiwa, na nitajitolea kuwatumikia watu na kuinua taifa, kukuza dini na maadili, na kueneza haki,"

Mkuu wa Idara ya Mahakama Gholam-Hossein Mohseni-Ejei aliendesha hafla ya kuapishwa.

Pezeshkian alianza rasmi muhula wake wa miaka minne siku ya Jumapili wakati Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei alipomuidhinisha kama rais kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa marudio wa Julai 5.Pezeshkian anachukua hatamu kutoka kwa mtangulizi wake, marehemu shahidi Rais Ebrahim Raisi, ambaye kifo chake katika ajali ya helikopta mwezi Mei kilisababisha uchaguzi wa mapema.

Baada ya kuapishwa, rais anatakiwa kisheria kuwasilisha orodha ya mwisho ya baraza lake la mawaziri Bungeni ili kuidhinishwa ndani ya wiki mbili.

Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kula kiapo cha kuwa rais, Pezeshkian aliutaka ulimwengu kutumia "fursa hii isiyo na kifani" ya kufanya kazi na Iran katika kukabiliana na changamoto za kikanda na kimataifa.

Rais alitoa wito wa ushirikiano wa kikanda ili kuunda eneo lisilo na ushawishi wa itikadi kali, akisema kuwa sauti za misimamo ya kufurutu ada hazipaswi kuwafunika karibu Waislamu bilioni mbili wanaopenda amani. Amesisitiza kuwa, "Uislamu ni dini ya amani."

Rais wa Iran pia alileleza matumaini yake kuwa kutakuwa ulimwengu ambapo "hakuna ndoto za mtoto wa Kipalestina zitazikwa chini ya vifusi vya nyumba zao."

Pezeshkian aidhe amezitaka nchi za Magharibi kuelewa ukweli wa mambo na kuwa na uhusiano na Iran kwa msingi kuheshimiana.


342/