Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limetangaza rasmi droni yake mpya ya kujitoa mhanga yenye injini ya ndege, iitwayo Hadid-110, inayotajwa kuwa ndiyo droni yenye kasi kubwa zaidi kuwahi kuzalishwa na Iran.

Kwa mujibu wa taarifa ya kijeshi, Hadid-110 imeundwa ili kuepuka mifumo ya rada na kutekeleza mashambulizi ya usahihi wa hali ya juu kwa kasi inayofikia kilomita 510 kwa saa (km/h). Droni hiyo imewekewa kichwa cha mlipuko chenye uzito wa kilo 30 na ina uwezo wa kufika umbali wa takribani kilomita 350.

Hadid-110 ilizinduliwa kwa kutumia mfumo wa reli unaosaidiwa na roketi, hali inayoiwezesha kufikia kasi ya juu mara baada ya kurushwa. Muundo wake wa kisasa unaojumuisha injini ndogo ya jet na umbo lenye pembe maalumu (low-observable faceted design) umeundwa mahsusi ili kupunguza uwezekano wa kugunduliwa na mifumo ya ulinzi wa anga.

Maafisa wa kijeshi wamesema kuwa droni hiyo inalenga kupenya ngome za ulinzi wa anga za adui na kushambulia malengo ya kudumu kwa muda mfupi wa onyo, jambo linaloipa uwezo mkubwa katika vita vya kisasa.

Taarifa zinaeleza kuwa mfumo huo tayari umejaribiwa katika mazoezi ya kijeshi, ishara inayoonyesha kuwa Iran inalenga kuiingiza kwa haraka katika matumizi ya kijeshi, kama sehemu ya kupanua na kuimarisha uwezo wake wa ndege zisizo na rubani (UAVs).

Hatua hii inaakisi mkakati wa Iran wa kuimarisha uwezo wake wa kujilinda na kuzuia vitisho vya nje, huku ikiendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kijeshi.

Your Comment