Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Dar es Salaam, Tanzania - Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Nchini Tanzania umeadhimisha kumbukumbu ya miaka 47 tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika hafla iliyohudhuriwa na mabalozi, maafisa wa serikali, wanadiplomasia na marafiki wa Iran nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Tanzania, Mohammad Javad Hemmatpanah, alieleza umuhimu wa Mapinduzi hayo na mafanikio ambayo Iran imeyapata katika kipindi cha zaidi ya miongo minne iliyopita. Alibainisha kuwa licha ya changamoto mbalimbali, Iran imepiga hatua kubwa katika sekta za sayansi na teknolojia, afya, elimu, viwanda pamoja na miundombinu.
Balozi Hemmatpanah alisifu uhusiano wa kihistoria na wa kirafiki uliopo kati ya Iran na Tanzania, akisisitiza kuwa mshikamano huo wa muda mrefu ni msingi imara wa kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali.
Aidha, alieleza utayari wa Iran kupanua ushirikiano wake na mataifa ya Afrika, hususan Tanzania, katika maeneo ya biashara, uwekezaji, uhamishaji wa teknolojia, kilimo na nishati. Aliongeza kuwa nchi hizi mbili zinaweza kunufaika zaidi kwa kuimarisha uhusiano wao wa kiuchumi na kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kibiashara.
Hafla hiyo ilikuwa pia fursa ya kuthibitisha dhamira ya pande zote mbili ya kuendeleza uhusiano wa kuheshimiana na kushirikiana kwa ajili ya maendeleo, amani na ustawi wa mataifa yao.
Your Comment