Main Title

source : Ripoti ya ABNA
Jumamosi

19 Machi 2011

20:30:00
265569

Makala zetu

Msikiti wa kwanza wajengwa Athens

Bunge la Ugiriki hatimaye limetoa kibali cha kujengwa msikiti wa kwanza mkuu mjini Athens, ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo, jambo ambalo limekuwa likijadiliwa kwa muda mrefu nchini humo.

Ripoti ya Shirika la Habari la Ahul Bayt(a.s)-ABNA- Ilieleza kuwa  kwa mujibu wa tovuti ya Hudson NY, bunge hilo lilipitisha mswaada wa kujengwa msikiti huo kwa sauti 198 kati ya sauti 300 za wabunge.

Kwa mujibu wa mswaada huo, serikali ya Athens inawajibika kuwajengea Waislamu sehemu ya kutekelezea kwa muda ibada zao katika kipindi cha miezi sita ijayo kabla ya kujengewa msikiti mkuu mwishoni mwa mwaka 2012 kwenye uwanja ulio na ukubwa wa mita mraba 1000.

Msikiti huo utakaokuwa na uwezo wa kupokea waumini 500 umetathminiwa kugharimu dola milioni 12.

Katika hali ya hivi sasa Waislamu wapatao laki tano wanakadiriwa kuishi nchini Ugiriki ambapo wengi wana asili ya Uturuki. Katika miaka ya hivi karibuni Waislamu kutoka Afrika, Asia ya Kati, Mashariki ya Kati na kusini mwa Asia wamekuwa wakihamia nchini humo kwa sababu tofauti. Wengi wa Waislamu laki mbili wanaoishi katika mji mkuu Athens pia wanatoka katika nchi za Afghanistan, Bangladesh, Misri, Nigeria na Pakistan.

Mgogoro wa kujengwa msikiti mkuu mjini Athens unarudi nyuma hadi katika miaka ya 1930. Mji wa Athens haujakuwa na msikiti mkuu na rasmi tokea utekwe na jeshi la Othmania mwaka 1833.