Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge katika Darsa ya Akhlaq amegusia moja ya maradhi hatari zaidi ya nafsi ya mwanadamu, nayo ni kibri (majivuno/maradhi ya kujiona bora). Kibri ni ugonjwa wa moyo unaomfanya mtu ajione bora kuliko wengine, kuwadharau, na kupuuza haki na ukweli. Katika mafundisho ya Kiislamu, kibri ni miongoni mwa sababu kuu zinazomwangusha mwanadamu kiroho na kijamii.
Maana ya Kibri
1-Kibri ni hali ya ndani ya moyo ambapo mtu:
2-Anajiona bora kuliko wengine
3-Anadharau watu wengine
4-Anakataa ukweli hata unapodhihirika wazi.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) amesema: "Kibri ni kuukataa ukweli na kuwadharau watu.”
Chanzo cha Kibri
Kibri hutokana na mambo kadhaa, miongoni mwao:
1-Elimu bila ikhlasi – mtu anapojiona msomi kuliko wengine
2-Mali na utajiri – kudhani mali humpa ubora
3-Nasaba na ukoo – kujivunia kizazi au kabila.
4-Cheo na mamlaka – kutumia nafasi vibaya.
5-Urembo na nguvu – kujiona bora kimwili.
Mifano ya kibri katika Qur’an ni kama Ibilisi, aliyekataa kumsujudia Adam (a.s) kwa sababu ya kibri, akisema:
“Mimi ni bora kuliko yeye; umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa udongo.” (Qur’ani 7:12).
Aina za Kibri
1-Kibri mbele ya Mwenyezi Mungu
– Kukataa amri za Allah na kujiona huru kutokana na utii.
2-Kibri mbele ya Mitume na Maimamu
– Kukataa mafundisho yao kwa sababu ya majivuno
3-Kibri mbele ya watu
– Kuwadharau maskini, wasio na elimu, au walioko chini kijamii
Athari za Kibri kwa Mwanadamu
Athari za Kiroho
Huua ikhlasi na unyenyekevu
Humfanya mtu apoteze hidaya
Hupelekea kuangamia Akhera
Humzuia mtu kutubia na kurejea kwa Allah
Imam Ali (a.s) amesema:
“Kibri ni ufunguo wa kila uovu.”
Athari za Kimaadili
Huzaa chuki, husuda na uadui
Humfanya mtu akatae ushauri
Humfanya mtu asiweze kujirekebisha
Athari za Kijamii
Hubomoa mshikamano wa jamii
Huleta migawanyiko na fitna
Huwafanya watu wamchukie mwenye kibri.
Athari za Kielimu
Msomi mwenye kibri hufungwa akili
Anakataa kujifunza kwa wengine
Elimu yake inakuwa chanzo cha upotofu badala ya nuru.
Dalili za Mtu Mwenye Kibri
Hapendi kukosolewa
Anajisifu kupita kiasi
Hudharau maoni ya wengine
Huwapenda watu wamsifia
Hukataa kukiri kosa.
Njia za Kujikinga na Kibri
1. Kujitambua Asili ya Mwanadamu
Kumkumbuka mwanadamu ameumbwa kwa udongo, tone la manii, na mwisho wake ni kaburi.
2. Kumkumbuka Allah Mara kwa Mara
Dhikri humfanya mtu ajione mdogo mbele ya Mola wake.
3. Kuwa Karibu na Wanyonge
Kukaa na masikini na wahitaji huvunja kibri.
4. Kujifanyia Muhasaba (Tathmini ya Nafsi)
Kujichunguza kila siku: Nimejivuna leo?
5. Kuomba Dua dhidi ya Kibri
Imam Sajjad (a.s) katika Dua ya Makaarimul Akhlaq anaomba:
“Ewe Mola, niondolee kibri moyoni mwangu.”
Mwisho Kabisa:
Kibri ni ugonjwa wa moyo unaoharibu uhusiano wa mwanadamu na Allah, watu, na hata nafsi yake. Kwa mwanafunzi wa Hawza, kibri ni hatari zaidi kwani huua baraka ya elimu na huzuia nuru ya maarifa kuingia moyoni. Njia ya wokovu ni unyenyekevu (tawadhu’), kwani Mwenyezi Mungu huwanyanyua walio wanyenyekevu na kuwashusha wenye kibri.

Your Comment