Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Sheikh Miraj Salim ameendelea na juhudi zake za kuimarisha elimu na uelewa wa masuala ya Kiislamu kupitia darsa za kila wiki zinazofanyika kila siku ya Alhamisi mjini Moshi, katika Msikiti wa Ahlul-Bayt (a.s).

Darsa hizi huendeshwa na Sheikh Miraj Salim, ambaye kwa mtindo wake wa kielimu na wenye mvuto huwasilisha mafunzo yenye kina yanayotokana na Qur’ani Tukufu na Sunna sahihi za Mtume wetu Muhammad (saww) na Watukufu wa Ahlul-Bayt (a.s).
Kupitia mihadhara hii, waumini hupata fursa ya kujifunza misingi ya itikadi, maadili ya Kiislamu, na mwongozo wa maisha unaojengwa juu ya haki, uadilifu na kumcha Mwenyezi Mungu.

Sheikh Miraj Salim hunukuu na kufafanua maneno ya Ahlul-Bayt (a.s) yanayosema: “Lau kama watu wangejua uzuri wa maneno yetu, wangelitufuata”, akisisitiza kuwa elimu sahihi ni ufunguo wa kuijua haki na kuifuata njia ya uongofu. Kauli hii imekuwa ni mwanga unaowahamasisha waumini kuzingatia elimu na kutafakari mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na kizazi chake kitukufu.

Waumini wanaoshiriki darsa hizi wameeleza kufaidika kwa kiwango kikubwa, wakibainisha kuwa mihadhara hiyo imewasaidia kuimarisha imani zao, kuongeza uelewa wa dini, na kujenga mshikamano wa kidini katika jamii ya Moshi na maeneo ya jirani.

Kupitia darsa hizi za kila wiki, ABNA inaendelea kutekeleza dhamira yake ya kueneza elimu sahihi ya Ahlul-Bayt (a.s), kuimarisha utamaduni wa kusoma na kujifunza, na kuandaa jamii yenye uelewa mpana wa mafundisho ya Kiislamu yanayolenga amani, maadili mema na maendeleo ya kiroho.

Your Comment