Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Ayatullah Sayyid Yasin Mousawi, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad na mhadhiri wa Chuo cha Kidini cha Najaf Ashraf, amesisitiza kuwa mchakato wa kisiasa nchini Iraq bado unakabiliwa na dosari ya kimuundo na ya kina; dosari inayodhihirika katika kukosekana kwa dhana ya kweli ya “serikali na upinzani”. Hali hiyo imesababisha mamlaka kubadilika kutoka “kuendesha nchi” na kuwa “kuendesha maslahi ya watu binafsi na makundi.”
Katika khutba ya Swala ya Ijumaa mjini Baghdad, Ayatullah Mousawi alisema: Elimu ya siasa inasisitiza uwepo wa mkondo unaotawala wenye dhamana ya kuendesha nchi, pamoja na mkondo wa upinzani unaofuatilia utendaji wa serikali na kurekebisha mwelekeo wake. Mfano huu, ukitekelezwa ipasavyo, unaweza kutibu makosa, kusahihisha sera, na hata—endapo uzembe utaendelea—kupelekea mabadiliko ya serikali kupitia njia za kisheria na kwa mujibu wa katiba.
Aliongeza kuwa mfumo huu ni mtindo wa kisayansi unaotambulika, kama ilivyo katika taaluma nyingine za sayansi ya jamii, lakini hali halisi ya kisiasa ya Iraq iko mbali sana na mtindo huo.
Akirejea mchakato wa kisiasa baada ya mwaka 2003, Imamu wa Ijumaa wa Baghdad alisema kuwa siasa za Iraq zilianza chini ya kile kilichoitwa “utawala wa uvamizi,” ambapo taasisi za mwanzo za serikali ziliundwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa mamlaka ya uvamizi ya Marekani.
Alibainisha kuwa mabadiliko ya kweli yalitokea pale Marjaa’iya ya juu ya kidini ilipoingilia kati na kusisitiza kuandaliwa kwa katiba kwa matakwa ya wananchi; katiba iliyothibitisha utambulisho wa taifa na misingi yake ya msingi, na kuweka msingi wa kuundwa kwa dola ya kitaifa inayopaswa kujengwa juu ya kanuni zilizo wazi za kikatiba.
Ayatullah Mousawi pia alirejea kipindi cha vurugu na ugaidi kilichoandamana na kile kilichoitwa “upinzani wa kisiasa,” akisisitiza kuwa wananchi wa Iraq walilipa gharama kubwa kwa damu ya watoto wao ili kushinda miradi ya umwagaji damu—iwe chini ya al-Qaeda au Daesh (ISIS).
Aliongeza: “Baada ya ushindi dhidi ya ugaidi, ilitarajiwa tuingie katika awamu ya ujenzi, lakini kwa masikitiko tumejikuta katika mgogoro mpya.”
Akikosoa vikali utendaji wa mikondo ya kisiasa, alisema kuwa Iraq haijawahi kuendeshwa kwa vitendo na vyama vyenye mipango ya kweli—wala vya Kiislamu wala vya kilimwengu - bali imekuwa ikiongozwa na watu binafsi wanaojificha nyuma ya majina ya vyama.
Alisisitiza: “Vyama vimeundwa kuwahudumia watu binafsi, si watu binafsi kuhudumia mipango ya kitaifa; na hili ndilo chanzo kikuu cha dosari.”
Imamu wa Ijumaa wa Baghdad alionya kuwa tishio kubwa zaidi kwa nchi leo ni pengo linalozidi kupanuka kati ya uongozi na wananchi—jambo ambalo Marjaa’iya ya juu ya kidini imekuwa ikionya juu yake mara kwa mara.
Alieleza kuwa chanzo cha mgawanyiko huo ni juhudi zisizoisha za kubaki madarakani na kunufaika na fursa zake, kiasi kwamba jukumu la kuongoza limegeuzwa kutoka “amana” na kuwa “nyara.”
Kuhusu mchakato wa kumchagua Waziri Mkuu, Ayatullah Mousawi alisema kuwa uwanja wa kisiasa unajirudia kwa mtindo uleule wa zamani: hakuna jina linalojadiliwa kwa misingi ya uwezo au mradi wa kitaifa, bali kipimo kimoja tu kinatawala—kulinda maslahi binafsi na kupata ridhaa ya Marekani.
Alisisitiza kuwa shinikizo za kiuchumi na kiusalama zinazowekwa na Washington haziwezi kamwe kuwa kisingizio cha kujisalimisha, iwapo kungekuwepo nia ya kweli ya kitaifa.
Akilinganisha hali ya Iraq baada ya zaidi ya miongo miwili tangu mabadiliko ya kisiasa na uzoefu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alisema: Iran imekuwa chini ya vikwazo vikali kwa miongo kadhaa, lakini licha ya hayo imefanikiwa kujenga dola imara katika nyanja za uchumi, kijeshi na teknolojia.
Aliongeza: “Sisi bado tunaagiza hata mahitaji yetu ya msingi, ilhali nchi zilizo chini ya mzingiro zinatengeneza silaha, viwanda na teknolojia. Tofauti ni kwamba huko kuna mfumo unaojiheshimu wenyewe na unaoheshimu watu wake.”
Ayatullah Mousawi alionya kuwa udhaifu wa utendaji wa kisiasa umeidhoofisha pia nafasi ya kimataifa ya Iraq, kiasi kwamba hata raia wa Iraq haheshimiwi kwa pasipoti yake—hali inayotokana na kukosekana kwa dola halisi na taasisi imara.
Alisisitiza kuwa taifa la Iraq ni kubwa na lenye subira, ambalo limethibitisha uwezo wake wa kustahimili hali ngumu zaidi—kuanzia zama za utawala wa zamani hadi vita vya ndani na ugaidi.
Alisema: “Taifa hili lina uwezo wa kutoa kafara kwa ajili ya nchi yake, lakini linahitaji uongozi wa kweli, wa kujitolea, na unaowaamini wananchi wake.”
Imamu wa Ijumaa wa Baghdad pia alikosoa kauli rasmi zinazozungumza kwa njia ya kuchagua kuhusu “kuheshimu matakwa ya wananchi,” akibainisha kuwa kura na matokeo ya uchaguzi mara nyingi huwekeza kupitia miungano ya kisiasa, si kwa misingi ya uungwaji mkono halisi wa wananchi. Alisema kuwa kuzungumza juu ya kuheshimu matakwa ya wananchi kunakuwa hakina maana pale ambapo wananchi wanaondolewa kivitendo katika mchakato wa maamuzi.
Mwisho wa khutba ya Swala ya Ijumaa, Ayatullah Mousawi alikataa kwa msimamo mkali mradi au makubaliano yoyote yanayodhoofisha mamlaka ya Iraq—ikiwemo miradi mikubwa ya uwekezaji inayokabidhiwa kwa nchi za kigeni na kulenga ardhi na maamuzi ya kitaifa. Alisisitiza kuwa miradi hiyo haitatekelezwa kamwe.
Alimalizia kwa kusema: “Iraq si nyara. Yeyote asiye na uwezo wa kubeba jukumu la uongozi anapaswa kukiri udhaifu wake, lakini kuigeuza dola kuwa bidhaa ya biashara ni aibu ya kisiasa.”
Imam wa Sala ya Ijumaa wa Baghdad:
"Chanzo cha dosari katika mchakato wa kisiasa wa Iraq ni kutanguliza maslahi binafsi na kujisalimisha kwa mashinikizo ya nje"
20 Desemba 2025 - 20:27
News ID: 1764078
Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Baghdad: Chanzo cha dosari katika mchakato wa kisiasa wa Iraq ni kutanguliza maslahi binafsi na kujisalimisha kwa shinikizo za nje
Your Comment