Main Title

source : Pars Today
Jumatano

12 Juni 2019

09:29:58
950173

Myanmar yakataa kuwapokea wakimbizi wa Rohingya

Waziri Mkuu wa Bangladesh amesema kuwa serikali ya Myanmar ndiyo inayopaswa kulaumiwa kwa kuchelewa kuwarejesha nyumbani wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya.

(ABNA24.com) Waziri Mkuu wa Bangladesh amesema kuwa serikali ya Myanmar ndiyo inayopaswa kulaumiwa kwa kuchelewa kuwarejesha nyumbani wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Bi Sheikh Hasina Wazed amesema kuwa tatizo ni kwamba Myanmar haitaki kuwapokea wakimbizi wa jamii ya Rohingya. Vilevile ameyakosoa mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu yaliyoko katika kambi za wakimbizi huko kusini mwa Bangladesh kwa sababu ya kukataa kuhamishwa kwa nguvu wakimbizi hao na kusema mashirika hayo hayataki kumalizwa kabisa mgogoro huo.

Hatua ya serikali ya Myanmar ya kukataa kurejeshwa nchini humo wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya ni ushahidi mwingine unaothibitisha kuwa, Mabudha wenye misimamo mikali wanaosaidiwa na jeshi la nchi hiyo wanaendelea kuwakandamiza na kuwamaliza taratibu na kwa mpangilio maalumu Waislamu wa jamii hiyo. Huu ndio ukweli ulioashiriwa mara kwa mara katika taarifa za Umoja wa Mataifa na kutaja mienendo ya serikali ya Myanmar dhidi ya jamii hiyo ya waliowachache kuwa ni jinai, uhalifu wa kupangwa na mauaji ya halaiki. Hata hivyo na licha ya kukiri katika ripoti zake kwamba yanayofanyika Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya ni jinai na uhalifu wa kupangwa, lakini Umoja wa Mataifa, kama zilivyo jumuiya nyingine za kimataifa na nchi za Magharibi, haujachukua hatua yoyote ya maana ya kuwarejesha wakimbizi hao nchini kwao. Suala hili pia limeashiriwa na Waziri Mkuu wa Bangladesh ambaye amesisitiza kuwa, jumuiya za kimataifa hazitaki kukomesha mgogoro wa wakimbizi wa Myanmar na kuhitimisha mgogoro wa nchi hiyo. 

Katika uwanja huo huo Abdul Aliim Mussa ambaye ni Imam wa Msikiti wa Islamu mjini Washington huko Marekani ameiambia televisheni ya Press kwamba: "Kimya cha nchi za Magharibi kuhusu mauaji ya kizazi yanayofanywa dhidi ya Waislamu wa Rohingya huko Myanmar ni kielelezo kwamba, maadili, familia, utamaduni na turathi za watu hazitakuwa na thamani yoyote kama hazidhamini vitu vinavyothaminiwa na nchi za Magharibi na kudhamini maslahi yao kama mafuta na dhahabu."

Ukweli ni kuwa, kimya cha nchi za Magharibi na uzembe na upuuzaji wa jumuiya za kimataifa mbele ya jinai zinazofanyika huko Myanmar kimekuwa sababu ya kuendelea mauaji ya kizazi cha Waislamu wa Rohingya na kuuhamasisha utawala wa Myanmar kukataa suala la kurejeshwa nyumbani wakimbizi wa jamii hiyo.

Robert Mardini ambaye ni miongoni mwa maafisa wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu nchini Myanmar amewaambia waandishi habari kwamba: 

"Hadi sasa hakujaandaliwa mazingira mazuri ya kuwafanya wakimbizi Waislamu wa Rohingya warejee nyumbani kwa hiari yao. Hakuna mtu anayeweza kudai kwamba, hali ya sasa huko Arakan inafaa kwa ajili ya kurejea salama wakimbizi wa Rohingya."

Novemba mwaka 2017 Myanmar na Bangladesh zilikubaliana juu ya suala la kurejeshwa nyumbani mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Rohingya lakini hadi sasa si tu kwamba, mwenendo wa kuwarejesha nyumbani wakimbizi zaidi ya laki saba walioko Bangladesh haujaanza lakini pia wakimbizi hao wenyewe hawana hamu ya kurejea makwao kutokana na ukatili unaoendelea kufanywa na Mabudha wenye misimamo mikali nchini kwao wakishirikiana na jeshi.

Suala hili limezidisha hali mbaya ya malaki ya wakimbizi Waislamu walioko Bangladesh na kuzidisha matatizo kwa nchi inayowapa hifadhi. Ni kwa sababu hii ndiyo maana serikali ya Bangladesh inatumia fusra zote zinazojitokeza kwa ajili ya kufikisha sauti yake kwa walimwengu ili watu wote duniani wafanye jitihada za kukomesha mgogoro huo na kuwalazimisha watawala wa Myanmar wawaruhusu raia hao Waislamu kurejea salama nchini kwao na kuwadhaminia usalama.



/129