Main Title

source : Pars Today
Jumatano

26 Juni 2019

08:57:12
955227

HRW: Saudi Arabia inapanga kumnyonga mtafiti Hassan al Maliki

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rigths Watch limetangaza kuwa utawala wa Saudi Arabia unakusudia kumhukumu na kumnyonga msomi na mtafiti maarufu Hassan Farhan al Maliki.

(ABNA24.com) Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rigths Watch limetangaza kuwa utawala wa Saudi Arabia unakusudia kumhukumu na kumnyonga msomi na mtafiti maarufu Hassan Farhan al Maliki.

Ripoti ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu imesema kuwa Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Riyadh anapanga mikakati ya kuitaka mahakama ya nchi hiyo itoe hukumu ya kifo dhidi ya msomi huyo kwa tuhuma zinazohusiana na fikra na mitazamo yake sahihi ya kidini.

Shirika la Human Rights Watch limeongeza kuwa, miongoni mwa tuhuma zinazomkabili ni eti kuwatukana watawala wa Saudi Arabia na kulitaja Baraza la Maulamaa wa nchi hiyo kuwa lina misimamo mikali.

Human Rights Watch imesema tuhuma hizo si makosa ya jinai yanayohalalisha adhabu ya kifo kwa mujibu wa sheria za haki za binadamu za kimataifa. imesisitiza kuwa kesi ya al Maliki inawasilishwa moja kwa moja katika ofisi ya mfalme wa nchi hiyo.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu pia limekumbusha kuwa ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Saudia inakusudia kuhimiza hukumu ya kifo dhidi ya msomi wa Kiislamu nchini humo, Sheikh Salman al Ouda kwa tuhuma za kutatanisha zinazohusiana na matamshi yake na msimamo yake ya kisiasa.

Miezi kadhaa iliyopita wanazuoni 80 wa Kiislamu wanaoishi katika nchi za Magharibi waliuandikia barua utawala wa kifalme wa Saudi Arabia wakiutaka usitekeleze hukumu ya kifo dhidi ya maulama watatu wa nchi hiyo wanaoshikiliwa gerezani. Maulama hao watatu ni Sheikh Salman al-Ouda, Sheikh Awad al-Qarni na Ali al-Omari.

Sheikh Salman al-Ouda alikamatwa na kufungwa jela mwaka 2017 baada ya kuandika ujumbe katika mtandao wa kijamii wa Twitter akisisitiza udharura wa kufanyika suluhu na mapatano baina ya Saudi Arabia na Qatar.Sheikh Awad al-Qarni ambaye ni mwandishi, mhubiri na mhadhiri wa chuo kikuu na mwenzake Ali al-Omari walitiwa nguvuni Septemba mwaka 2017.

Tangu Muhammad bin Salman alipoteuliwa kuwa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia tarehe 21 Juni mwaka 2017 maulama, wasomi na wanaharakati wa masuala ya kijamii wamekuwa wakikabiliwa na mbinyo na ukandamizaji mkubwa nchini humo. Ripoti zinasema kuwa tangu mwezi Septemba mwaka 2017 hadi Septemba 2018 askari usalama wa Saudia wamewatia nguvuni zaidi ya maimamu na mahatibu mia moja wa misikiti nchini humo.



/129