Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Tangu jana Alkhamisi wanaharakati hao wamekuwa wakitaja visa vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu, dhulma, ufisadi wa watawala wa Saudi Arabia na kukosoa matatizo ya kiuchumi, ongezeko kubwa la nakisi ya bajeti, mdodoro wa uchumi na ukosefu wa ajira nchini humo.
Wanaharakati wa mitandao ya kijamii wa Saudia pia wametangaza kuwa Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu hauwezi kukombolewa bila ya kwanza kuporomoka utawala wa Aal Saudi na kukombolewa Makka na Madina.
Wakati huo huo na sambamba na kuachiwa huru mwanaharakati wa kike wa Saudia, Loujain al-Hathloul, kutoka kwenye jela ya Saudia, taasisi na jumuiya mbalimbali zimezidisha mashinikizo dhidi ya serikali ya Riyadh zikitaka kuachiwa huru wafungwa wote wa kisiasa nchini humo.
Baada ya kuachiwa huru Loujain al-Hathloul amesema kuwa ana azma ya kuwafungulia mashtaka wale wote waliohusika katika kuteswa kwa nyaya za umeme, kupigwa bakora na kunajisiwa kwake.
Loujain al-Hathloul mwenye umri wa miaka 32 alishikiliwa jela nchini Saudi Arabia tangu mwezi Mei mwaka 2018. Mwanaharakati huyo wa kike alikamatwa na kufungwa jela kwa sababu ya kudai uhuru wa mwanamke kuendesha gari Saudi Arabia. Hata hivyo mwendesha mashtaka wa serikali ya nchi hiyo alimbambikia tuhuma za kusababisha madhara kwa maslahi ya taifa. Mwezi mmoja baadaye, Saudia iliwapa wanawake haki na kuendesha magari. Hata hivyo Loujain al-Hathloul aliendelea kusota jela kwa kipindii cha zaidi ya miezi 30.
Katika kipindi chote hicho mwanaharakati huyo hakufikishwa mahakamani hata mara moja na aliendelea kushikiliwa bila ya kuhukumiwa. Mbali na hayo Loujain alikabiliwa na sulubu na mateso mengi katika jela ya serikali ya Saudia. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametangaza kuwa, Loujain al-Hathloul alipewa mateso ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuteswa kwa kutumia nyaya za umeme na kunajisiwa.
Katika ripoti yake iliyopewa anwani ya "Jahannam ya kila siku ya mwanaharakati wa kike wa Saudi katika jela", gazeti la Uingereza la Independent liliandika kuwa: "Loujain al-Hathloul anaishi katika mazingira ya Jahannam kwenye jela ya Saudi Arabia na amelazimika kugoma chakula kwa wiki kadhaa akilalamikia mazingira hayo."
342/