21 Oktoba 2022 - 16:43
Watu wasiopungua 50 wauawa katika maandamano ya umwagaji damu nchini Chad

Takriban watu 50 wameuawa na karibu wengine 300 kujeruhiwa katika ghasia zilizozuka nchini Chad hapo jana baada ya mamia ya watu kuingia mitaani kudai mabadiliko ya haraka kuelekea utawala wa kidemokrasia.

Saleh Kebzabo, Waziri Mkuu wa Chad ambaye alitangaza idadi ya waliouawa katika mkutano na waandishi wa habari, amesema kuwa serikali bado inakusanya takwimu za idadi ya majeruhi kutokana na kile alichokitaja kuwa ni uasi wa kutumia silaha.

Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa raia wasiokuwa na silaha waliuawa huku vikosi vya usalama vikikabiliana kikatili na maandamano katika mji mkuu N'Djamena na miji mingine kadhaa ya nchi hiyo.

Taifa hilo kubwa la Afrika ya Kati linalotawaliwa na jeshi limekuwa katika mgogoro tangu kifo cha Aprili 2021 cha Rais Idriss Deby, ambaye alitawala kwa mkono wa chuma kwa miongo mitatu.

Mahamat Idriss Deby

 

Mtoto wake wa kiume, Mahamat Idriss Deby, alinyakua madaraka mara moja na awali aliahidi kipindi cha mpito cha miezi 18 kuelekea uchaguzi, lakini Oktoba mosi alitangaza kwamba watasogeza mbele kwa miaka miwili.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Rais wa serikali ya mpito ya Chad ametangaza hali ya hatari kufuatia mvua kubwa na mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo.

Rais wa serikali ya muda ya Chad, Mahamat Idriss Déby Itno, ametangaza hali ya hatari kutokana na mafuriko yaliyotokea nchini humo, ambayo yamesababisha uharibifu na hasara kwa watu zaidi ya milioni moja.

Kwa kawaida, mvua za masika hunyesha nchini Chad kuanzia mwezi Mei na kuendelea hadi Oktoba; lakini mwaka huu, mvua hizo zimekuwa kubwa mno kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa iliyopita.

342/