25 Juni 2026 - 18:50
Mahakama ya Damascus Yaanza Kesi dhidi ya Aliyekuwa Mufti wa Syria, Ahmad Hassoun, kwa Tuhuma za Kuhamasisha Uhalifu wa Kivita

Mahakama ya Jinai ya Nne mjini Damascus imeanza kusikiliza kesi dhidi ya aliyekuwa Mufti wa Jamhuri ya Syria, Ahmad Hassoun, anayekabiliwa na tuhuma za kuchochea mauaji, kuhalalisha uhalifu wa kivita na kutoa uungwaji mkono wa kidini na kisiasa kwa utawala wa zamani wa Bashar al-Asad na washirika wake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s.) –ABNA–, Mahakama ya Jinai ya Nne mjini Damascus, Syria, imefanya kikao chake cha kwanza cha kusikiliza kesi dhidi ya aliyekuwa Mufti wa Jamhuri ya Syria, Ahmad Hassoun, mbele ya Mwanasheria Mkuu Hassan al-Turba na kwa kuhudhuriwa na mashirika ya ndani na ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu.
 
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na Jaji Fakhruddin al-Aryan, Ahmad Hassoun anatuhumiwa kutumia nafasi yake ya kidini kwa manufaa binafsi, kujenga uhusiano wa karibu na viongozi wa utawala wa zamani wa Bashar al-Assad, maafisa wa usalama, makamanda wa jeshi na viongozi wa makundi yaliyoshiriki katika vita vya Syria.
 
Mashtaka hayo pia yanamhusisha na kutoa hotuba na matamshi ya hadharani yaliyodaiwa kuwahamasisha wanajeshi wa utawala wa zamani kuendelea na mapambano dhidi ya wapinzani wao, pamoja na kutoa kauli zilizotafsiriwa kuwa ni uchochezi dhidi ya raia katika maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na waasi, hususan Aleppo Mashariki na Idlib.
 
Mahakama imeeleza kuwa matendo yanayodaiwa kufanywa na Hassoun yanaweza kumfanya kuwa mshiriki katika uchochezi, msaada wa kimaadili na utoaji wa uhalali wa kidini kwa vitendo vinavyochukuliwa kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
 
Mwakilishi wa Ofisi ya Mashtaka, Jaji Omar al-Radhi, amesema kuwa kesi hiyo haihusu mtu wa kawaida, bali mtu aliyekuwa na nafasi ya juu ya kidini ambayo ilipaswa kuwa chombo cha kuhimiza amani na kuzuia umwagaji damu.
 
Aidha, upande wa mashtaka umedai kuwa Ahmad Hassoun alitumia nafasi yake kama Mufti wa Aleppo na baadaye Mufti wa Jamhuri ya Syria kujenga mtandao wa mahusiano na viongozi wa utawala wa zamani, huku akihusishwa na kauli na matamshi yaliyotafsiriwa kuwa ni uchochezi dhidi ya wapinzani wa serikali na waandamanaji.
 
Kesi hiyo imevutia hisia za ndani na kimataifa, huku ikichukuliwa kuwa miongoni mwa kesi muhimu zinazohusiana na kuwajibishwa kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa na kidini kwa matukio yaliyojitokeza wakati wa mzozo wa Syria uliochukua zaidi ya muongo mmoja.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha