Mbali na lugha ya Kiswahili, mtandao wa habari na utamaduni wa "parstoday.com" una lugha nyingine 24 kwa ajili ya kuwapa habari za uhakika watu wa kona mbalimbali za dunia. Lakini nchi za Magharibi ambazo zinadai ni viranja wa demokrasia na uhuru wa kusema, zimeshindwa kuvumilia kusikia maoni na sauti ya upande wa pili, na zimeamua kuufungia mtandao huo ikiwa ni sehemu ya vikwazo vya kidhalimu vya madola ya kibeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Shirika linalotoa huduma za domain ya ".com" limedai kuwa, Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) limewekewa vikwazo na Marekani, Umoja wa Ulaya na Canada, hivyo shirika hilo nalo limeamua kusitisha huduma zake kwa IRIB.
Mkuu wa Kitengo cha Matangazo ya Ng'ambo cha IRIB amelaani hatua hiyo na kusema kuwa, sasa mtandao wa parstoday utakuwa unapatikana kwa domain ya ".ir" yaani parstoday.ir. Hii ikiwa na maana kwamba, tovuti ya Idhaa ya Kiswahii Radio Tehran nayo itakuwa inapatikana kwa "parstoday.ir/sw."
Mtandao wa habari, utamaduni na redio wa parstoday ulianza kufanya kazi rasmi mwaka 2015 ukisambaza habari zake kwa lugha tofauti kama Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kichina, Kijapani n.k. Umekuwa ukirusha hewani matangazo yake kwa lugha tofauti kwa saa 24 kwa siku kwa ajili ya wasikilizaji wa kona zote duniani.
Nchi za Magharibi yaani Marekani, Umoja wa Ulaya na Canada zinasema uongo wa wazi zinapodai kuwa ziko huru na ziko tayari kusikiliza mitazamo na maoni ya upande wowote ule. Satalaiti ya Eutelsat nayo siku ya Alkhamisi ya tarehe 22 Disemba 2022 ilizifungia kanali zote za redio na televisheni za IRIB zisirushe matangazo yake kupitia satelaiti hiyo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani amesema, hatua ya nchi za Magharibi ya kufungia matangazo ya IRIB na televisheni ya Press TV imelenga kuzuia kuwafikia walimwengu sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na huko ni kuendelea kukanyaga waziwazi haki za taifa la Iran na haki za walimwengu za kupata taarifa kutoka pande tofauti, kwa uhuru na uwazi.
342/