17 Julai 2024 - 19:08
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa: Kila eneo la Gaza ni uwanja wa mauaji

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, mashambulizi na jinai zinazoendelea kufanywa na jeshi la utawala ghasibu wa Israel katika kambi za wakimbizi wa Kipalestina huko Ukanda wa Gaza vimegeuza kila sehemu ya eneo hilo kuwa uwanja wa mauaji.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, kiasi cha uharibifu katika Ukanda wa Gaza hakitasawariki wala hakikubaliki, na hakuna sehemu salama katika Ukanda wa Gaza.

Antonio Guterres ametoa wito kwa pande zote kuonyesha ujasiri na kutangaza nia yao ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.

Awali, Inas Hamdan, mkurugenzi wa Ofisi ya Habari ya Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) katika Ukanda wa Gaza, alisema tangu kuanza kwa vita, vituo 190 vya wakala huo wa Umoja wa Mataifa vimeharibiwa katika mashambulizi ya Israel.

Inas Hamdan amesema, inasikitisha kwamba, hakuna eneo salama katika Ukanda wa Gaza, na wakimbizi wa Kipalestina hawawezi kupata maeneo salama ya kupita na kuondoka Ukanda wa Gaza.

Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, utawala wa kikatili wa Israel, ukiungwa mkono kikamilifu na nchi za Magharibi, ulianzisha mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan dhidi ya watu wasio na ulinzi na madhulumu wa Palestina.

Takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza zinasema, zaidi ya Wapalestina elfu 38 wameuawa shahidi na zaidi ya wengine elfu 88 wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

342/