Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Maosud Pezeshkian mjini New York kama Rais wa Iran. Amekwenda New York kushiriki katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na mikutano yake ya pembeni ni muhimu sana kwa serikali za ulimwengu.
Viongozi na wawakilishi wakuu wa serikali hujaribu kutumia fursa ya mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na mikutano yake ya pande kadhaa na ya pande mbili kuwasilisha maoni yao kuhusu masuala muhimu zaidi ya kimataifa na kikanda na mitazamo ya serikali zao.
Kwa viongozi ambao hivi karibuni wamechaguliwa kuongoza nchi zao, kushiriki katika mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuna umuhimu maradufu.
Nukta hii inapata umuhimu hasa kwa nchi kama Iran ambayo iko katika nafasi muhimu ya kijiografia na kikanda. Baada ya kuwasili New York, katika hotuba yake ya kwanza katika mkutano wa Mkataba wa Mustakabali kwa ajili ya maendeleo ya nchi na kuleta amani na usalama, katika kikao hicho, Rais wa Iran ameeleza na kufafanua wazi sera za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Rais wa Iran amesema katika kikao hicho kwamba kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo kunahitaji ushirikiano na maingiliano yanayozingatia uadilifu na ukweli. Ameongeza kuwa: “Njooni tutengeneze mustakabali wa haki na ustawi kwa watoto wetu; Lengo la juhudi hizi za pamoja ni kutilia maanani nafasi na hadhi ya Umoja wa Mataifa kama nembo ya ushirikiano wa pande kadhaa na kuheshimu malengo na kanuni za hati yake. "Pezeshkiana ameongeza kuwa: "Tunataka marekebisho ya haraka katika muundo wa utawala na taasisi za fedha za kimataifa ili kujumuisha nchi zinazoendelea katika muundo wa maamuzi."
Jumapili, Septemba 22, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha mpango unaoitwa "Mkataba wa Mustakabali."Mkataba huo unaleta pamoja mataifa yanayozidi kugawanyika duniani ili kukabiliana na changamoto za karne ya 21, kuanzia mabadiliko ya hali ya hewa na Akili Mnemba hadi migogoro inayoongezeka na kushadidi kwa ukosefu wa usawa pamoja na kukithiri umaskini duniani.
Katika hotuba yake ya kuimarisha malengo ya Umoja wa Mataifa Rais Pezeshkian amesema: "Kuimarishwa mfumo wa kuchukuliwa maamuzi na pande kadhaa ili kukabiliana na changamoto kama vile vita, umaskini, ubaguzi na njaa unapaswa kuwa msingi wa kazi ya pamoja katika siku zijazo."
342/