22 Desemba 2024 - 15:06
Dini ya Mtume (s.a.w.w) kabla ya Utume (Biitha) wake

Nabii Muhammad (s.a.w.w) hakufuata Dini ya Nabii Ibrahim (a.s), wala Dini ya Nabii Musa (a.s), wala Dini ya Nabii Issa (a.s); bali yeye alikuwa na Wajibu (Taklif) mahsusi kwake mwenyewe binafsi, na Malaika walikuwa wakimfikishia matendo na ibada za waja na mienendo ya Kidini kwa njia ya Wahyi, na njia (namna) ya ibada na uja wa Mtume ilikuwa ni kufuata maamrisho aliyoyapokea kwa njia hii.

Katika muda wa miaka arobaini, Mtume (s.a.w.w) alitenda hivyo hivyo, mpaka alipochaguliwa kuwa Mtume; na kutumwa (Biitha) kama Mjumbe (wa Allah) akiwa na umri wa miaka arobaini.

Shirika la Habari la Ahl al-Bayt (a.s) / Abna:

Swali: Je, ni Dini gani ya Mtume (s.a.w.w) kabla ya (Biitha) Utume wake?.

Jibu: Hadhrat Muhammad (s.a.w.w) alitumwa kama Nabii akiwa na umri wa miaka arobaini (40) na kama Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, aliwaita watu kwenye njia iliyonyooka.

Hata hivyo, kumekuwa na tofauti ya maoni kuhusu ni Dini gani ambayo yeye mwenyewe aliifuata kabla ya kutumwa na kupewa Utume (kabla ya kuchaguliwa kuwa Mtume), na wameeleza mambo matatu yanayowezekana (kwamba kuna ihtimali Tatu kuhusu Dini yake ya Biitha yake): Dini iliyonyooka (Dini ya Nabii Ibrahim a.s), Dini ya Ukristo, na Dini ya Uislamu.

Dini ya Kiyahudi ilikomeshwa na mwanzo wa Utume wa Yesu / Issa (a.s), na alitangaza mwisho wa Sheria ya Musa (a.s) kwa kuleta Dini ya Umasihi - au Unaswara - (Ukristo). Ukristo (Unaswara) ni Dini ya mwisho ambayo Mwenyezi Mungu aliituma kwa wakazi wa Dunia hii kabla ya Uislamu, na haikufutwa hadi ujio wa Uislamu.

Kwa hiyo, uwezekano wa kwanza (ihtimali ya kwanza) kuhusu Dini ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni Ukristo (Unaswara).

Ikiwa nadharia ya mageuzi (mabadiliko) ya Dini itakubaliwa, uwezekano huu unaimarishwa zaidi, kwa sababu kulingana na nadharia hii, Dini ya Unaswara ya Yesu / Issa (a.s) ilikuwa Dini kamilifu zaidi hadi wakati huo.

Lakini uwezekano huu unakabiliwa na matatizo, kwa sababu Dini yenyewe ya asili ya Yesu Kristo (Issa bin Maryam) (a.s) -Dini halisi ya Unaswara - ; ambayo ilikuwa katika ngazi ya juu kuliko Dini nyingine zote, haikuwepo wakati wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwa sababu ilipotoshwa kabisa na mtu aitwaye Paulo.

Suala jengine linalokanusha Mtume Muhammad (s.a.w.w) kuwa katika Dini ya Umasihi (Unaswara au Ukristo); ni nadharia iliyopo kwamba Ukristo si wa ulimwengu wote (haikuwa Dini ya Kila eneo la Ulimwengu), kwa sababu wengine wanamchukulia Yesu / Issa bin Maryam (a.s) kuwa nabii aliyelelewa kwa ajili ya Wana wa Israel tu, si kwa ajili ya Wanadamu wote (popote walipo Ulimwenguni). Kwa hivyo, si rahisi kuthibitisha kuwa hiyo ilikuwa Dini ya Ulimwengu wote.

Pia, sababu nyingine ya kukataa hali ya Ukristo kuwa ndio Dini ya Mtume (kabla ya Biitha) ni kwamba: Hakuna mtu yeyote katika historia aliyedai kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuwa akifuata Ukristo (Dini ya Umasihi au Unaswara); pia, hakuna ushahidi wa uwepo wa Mtume (s.a.w.w) katika Kanisa kwa ajili ya ibada. Dini iliyotangulia, Uyahudi, pia haikuwa salama kutokana na upotoshaji, na hakuna yeyote katika historia aliyemchukulia Mtume Muhammad (s.a.w.w) kama Muumini wa Uyahudi.

Kwa hiyo, wengine wanaamini kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuwa wa Dini ya Nabii Ibrahim (a.s).

Kwa mujibu wa nadharia hii, ni kweli kwamba Jahiliyyah ya Waarabu (kwa maana: Waarabu wa Zama za Kijahiliyyah / za Ukafiri), waliikengeusha Dini ya Nabii Ibrahim (a.s) na kuielekeza kwenye upotovu (na upotoshaji), na kuchanganya ibada za Dini ya Ibrahimu (a.s) na Ushirikina wa Kijahiliyyah.

Ama Dini hii ya Safi (na iliyonyooka ya Nabii Ibrahim a.s), haikupotoshwa ndani yake kutoka kifua hadi kifua cha Mababu wa Mtume Muhammad (rehema na amani ziwe juu yake na Aali zake), mpaka kumfikia Mtume huyu (s.a.w.w).

 Kwa mantiki hiyo, tunaweza kuona kuwa kiwango cha ukamilifu wa Dini ya Kikristo (Umasihi) katika zama za Mtume (rehema na amani ziwe juu yake na Aali zake) ni chini zaidi ukilinganisha na Dini Hanif / Safi na iliyonyooka ya Ibrahim (a.s) iliyokuwa vifuani mwa Wafuasi wa Dini hii, yaani Wafuasi wa Dini ya Ibrahim (a.s) katika Mji wa Makkah.

Kwa sababu Dini asili ya Ukristo (Umasihi - Unaswara ambao haujapotoshwa) haikuwepo baina ya watu kwa wakati huo, na ni muhimu kufuata Dini asili na halisi (ambayo haijatiwa upotoshwaji), ujuzi wa mafundisho ya Dini hii ni muhimu, na kwa uwepo wa Injili (Biblia) zilizopotoshwa, inakuwa haiwezekani kamwe kufuata Sharia ambayo Yesu / Issa (a.s) aliileta hapo mwanzo (kwa sababu sio rahisi kutambua lipi sahihi na lipi sio sahihi baada ya mikono ya wapotoshaji kutia upotosha ndani yake).


Nadharia ya kuwa Mtume (s.a.w.w) alifuata Dini ya Ibrahim (a.s) inatokana na baadhi ya Aya za Qur’an Tukufu, ikiwa ni pamoja na:

"Kisha tukakuteremshia Wahyi ili ufuate Mila (Dini) ya Ibrahim, ambayo haikuwa na aina yoyote ile ya upotofu, na wala hakuwa - Ibrahim - miongoni mwa washirikina".

Vile vile Aya isemayo:

“Sema, Mola wangu Mlezi ameniongoza kwenye njia iliyonyooka, Dini yenye kudumu na yenye kudhamini furaha ya Dini na Dunia, Dini ya Ibrahim, aliyejitenga na dini za kishirikina za mazingira yake (zilizokuwa zimemzunguka), na hakuwa miongoni mwa washirikina."

Hata hivyo, kufuata Dini ya Hanif (Dini iliyonyooka ya Nabii Ibrahim a.s) pia kunakabiliwa na matatizo ishkalati kadhaa), kwa sababu Aya hizo hapo juu ziliteremshwa baada ya (Biitha) Utume wa Mtume na hazirejelei Dini ya Mtume (s.a.w.w) katika kipindi cha kabla ya (Biitha) Utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), na huenda / inawezekana kusema kuwa makusudio ya kumfuata Hadhrat Ibrahim (a.s) ni kufuata katika Njia ya Hadhrat Ibrahim (a.s) iliyobakia, na si kufuata katika kila (kipengele na kila) sehemu ya Sharia.

Uwezekano mwingine (ihtimali nyingine) ni kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuwa akitekeleza Wajibu (Taklif) ulioegemezwa juu ya Wahyi (aliokuwa akiupokea) kabla ya (Biitha) Utume wake. Kwa msingi wa uwezekano huu, Dini ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) kabla ya Biitha yake iliwasiliana na Malaika wa Wahyi, ambapo alikuwa akipokea Maelekezo ya Taklif zake moja kwa moja kutoka Malaika wa Wahyi, na kuna riwaya kadhaa zinazothibitisha nadharia hii.

Katika kuunga mkono nadharia hii, Hadhrat Ali (a.s) anasema:

"Tangu siku Mtume (s.a.w.w) alipoachishwa kunyonya, Mwenyezi Mungu alimuwekea Swahiba na Rafiki wa karibu zaidi, na Malaika mkubwa zaidi, ili kupitia Malaika huyo, aweze kupata ukuu na kupambwa kwa Akhlaq na maadili bora zaidi".

Pia imesemwa katika riwaya nyingine:

“Jua! Wanavyuoni wanakubaliana kwamba Mtume (s.a.w.w) alikuwa akiswali na kufunga kwa siri, kinyume na ilivyoonekana katika matendo na ibada za kabila la Makuraishi, kabla ya (, Biitha) Utume wake, na tokea alipofikia Taklif yake (Kutumwa kuwa Mtume) akiwa ni mwenye umri wa miaka 40, na Mwenyezi Mungu akamuamuru Malaika Jibrail (a.s) amshukie na kumpa Ujumbe wa (Biitha) kuteuliwa kuwa Mtume / Mjumbe (wa Allah).

Kwa hiyo, kama vile ilivyo kwa mujibu wa Aya ya Qur'an, Yesu / Issa (a.s) alipewa kitabu akiwa mtoto; Hadhrat Muhammad (a.s) pia alikuwa akiwasiliana na Ulimwengu wa Wahyi tangu mwanzo kabisa wa maisha yake (akiwa Mtoto), na alipofika katika Umri wa miaka arobaini (40) alitumwa kuitangaza (kuineza) Dini yake kwa kila mtu.

Wengine wamedai (ijmaa) makubaliano juu ya nadharia hii na wanaikubali.

Maoni ya Sheikh Tusi kuhusu hili ni kama ifuatavyo:

“Tunaamini kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) hakufuata Sheria yoyote ya Mitume wa kabla yake, si kabla ya (Biitha) Utume wake wala baada ya Utume wake; bali ukweli ni kwamba, kila tendo (lolote) la ibada alilolifanya lilionwa kuwa ni makhsusi kwake na kuhesabiwa (kuchukuliwa) kuwa ni Sharia.

Kwa mantiki hiyo, baadhi ya Wanachuoni / Wanazuoni wetu wanaamini kuwa kabla ya Biitha ya Mtume (Kabla ya kutumwa kuwa Mtume), alikuwa akipewa Wahyi wa kuelekezwa namba ya kufanya ibada (zake), ambazo zilikuwa ni maalumu na makhsusi kwake, na yeye pia alikuwa akitekeleza Wahyi huo, lakini (Maelekezo hayo) hayakuwa katika namna au mlango wa kufuata Sharia ya kabla yake.

Anaendelea kusema:

“Ushahidi wetu kwa madai yetu ni maafikiano ya Wanachuoni wa Madhehebu ya Haki juu ya suala hili na kutokuwepo ikhtilafu yoyote ndani yake, na sababu yetu nyingine ni kwamba imethibiti kwa maafikiano kwamba yeye (Hadhrat Muhammad) ni mbora wa Manabii wote waliopita kabla yake (waliomtangulia). Kwa hiyo, haijuzu kwa Mwenyezi Mungu kuamrisha aliye bora zaidi kumtii na kumfuata aliye chini yake kwa ubora, na hili ni jambo ambalo tumelisisitiza mara kadhaa".

Al_Allamah Al_Hilli pia anasema kuhusiana na hili:

“Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) hakuwa mfuasi wa Sharia yoyote kabla yake, si kabla ya (Biitha) Utume wake wala baada ya Utume wake, na lau ingelikuwa kinyume na hilo (kuwa alifuata Sharia yoyote ya kabla yake), basi hilo lingejipatia umaarufu (lingekuwa ni jambo mashuhuri), na (tungeliona kokote) watu wa Sharia hiyo wakijivunia na kujifakharisha kwa hilo, na pia ingelikuwa ni muhimu (ni lazima) kwake kurejelea mara kwa mara (katika Sharia hiyo) na kupata majibu ya maswali yake kutoka kwake".

Inaonekana kwamba natija aliyoifikia Allamah Majlisi kwa mujibu wa riwaya zote hizo, ndio kauli sahihi na rai iliyo sahihi zaidi. Anasema:

“Mtume (s.a.w.w.) alikuwa na Nafasi ya Utume (Mwenye kustahili Daraja ya Utume) kabla ya Nafasi ya Unabii (kabla ya Kustahili Daraja ya Unabii), wakati mwingine Malaika walikizungumza naye na alikuwa akisikia sauti zao, na wakati fulani alipokea Wahyi wa Mwenyezi Mungu katika ndoto ya kweli, na baada ya miaka arobaini (40), alifikia Nafasi (Daraja) ya Utume (Daraja ya kutumwa kuwa Mtume); na hapo Qur'an na Uislamu viliteremshwa rasmi kwake".

_

Vyanzo:

1. Durant, William James, Historia ya Ustaarabu (History of civilization / Tareikh Tamaddun), Juzuu 1, Watarjumu: Leila Zare, Hossein Ghayab, Mohammad Amin Alizadeh, Tehran: Behnoud Publications, 1393 Hijria Shamsiyyah, Juzuu 3, uk. 689 na 697.

2. Subhani, Mafahimul Qur'an, Qom, Taasisi ya Imam Sadiq, 1413 AH, Juzuu ya 3, uk.73 na kuendelea.

3. Surah Nahl, Aya ya 123.

4. Surah An'am, Aya ya 161.

5. Mudhafari, Muhammad, Maswali na Majibu, Qom, Umm Abiha, 1420 AH, uk.12.

6. Al_Kulayni, Muhammad bin Yaqub, Al-Kafi, utafiti na marekebisho ya Ali Akbar Ghafari na Muhammad Akhundi, Tehran, Dar al-Kitab al-Islamiya, 1407 AH, juzuu ya 2, uk.17.

7. Majlisi, Muhammad Baqir bin Muhammad Taqi, Bihar al-Anwar, Beirut, Dar Ihya al-Tarath al-Arabi, 1403 AH, juzuu ya 18, uk.266.

8. Majlesi, Muhammad Baqir bin Muhammad Taqi, Bihar al-Anwar, Beirut, Dar Ihya al-Tarath al-Arabi, 1403 AH, juzuu ya 18, uk.278.

9. Fatal Nishabouri, Muhammad bin Ahmad, Roza al-Wa'zin na Basira al-Mu'ta'zin, Qom, Razi Publishing House, 1375, uk.52.

10. Surah Maryam, aya ya 12 na 13.

11. Mudhaffar, Mohammad Hossein, "Ilmu Imam", iliyotafsiriwa na Mohammad Asefi, Tabriz, 1349, uk.76 na kuendelea.

12. Sheikh Tusi, Adah al-Asul, juzuu ya 2, uk.590.

13. Allamah al-Hilli, al_Wusul, uk.170.

14. Majlisi, Muhammad Baqir bin Muhammad Taqi, Bihar al-Anwar, Beirut, Dar Ihya al-Tarath al-Arabi, 1403H, Juzuu ya 28. Uk. 288.