26 Desemba 2024 - 05:21
Indhari Ujerumani kuhusu chuki dhidi ya Uislamu kufuatia shambulio la Krismasi

Kamishna wa Shirikisho la Kupambana na Ubaguzi nchini Ujerumani, Reem Alabali-Radovan, ameelezea wasiwasi wake siku ya Jumatatu kuhusu kuongezeka kwa chuki na mashambulizi dhidi ya Uislamu kufuatia tukio la hujuma kwa kutumia gari katika soko la Krismasi huko Magdeburg wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu 5 na kujeruhi wengine 200.

Alabali-Radovan alisema kuwa vituo vya ushauri dhidi ya ubaguzi wa rangi huko Magdeburg na mikoa ya jirani vimeripoti kuongezeka kwa uhasama na ghasia zinazowalenga wahamiaji na Waislamu tangu tukio hilo.

 "Kwa bahati mbaya, kitendo hiki sasa kinatumika kama njia ya kuruhusu ubaguzi wa rangi kuendelea. Hatupaswi kukubali hilo kwa hali yoyote. Lazima tupinge jaribio lolote la kutumia kitendo hiki kisiasa.”

Alisisitiza kuwa vitendo vya ugaidi vinalenga kuvunja umoja wa kijamii, kuzusha hofu na kuleta mgawanyiko ndani ya jamii.

Makamu wa Kansela wa Ujerumani Robert Habeck pia alihutubia taifa mapema mchana, akiwataka raia kutokubali chuki au habari potofu zinazosambazwa mitandaoni.

Mshambulizi anayeshukiwa, aliyetambuliwa kama Taleb Al-Abdulmohsen, daktari wa akili mwenye umri wa miaka 50 kutoka Saudi Arabia, alikuwa akiishi Ujerumani tangu 2006 na alikuwa ameajiriwa huko Bernburg, mji ulio kusini mwa Magdeburg.

Mamlaka zimefichua kuwa Abdulmohsen alikuwa na misimamo dhidi ya Uislamu, kwani alisharitadi,  na amekuwa akiunga mkono itikadi kali za mrengo wa kulia, ikiwa ni pamoja na kusambaza taarifa za kupendelea chama cha Mbadala kwa ajili ya Germany (AfD) ambacho kinajulikana kwa misimamo yake dhidi ya Waislamu.

IQNA