Mohammad Baqer Qalibaf, ameyasema hayo leo katika hotuba aliyotoa kabla ya kuanza kikao cha kawaida cha Bunge la Iran na akabainisha kwamba, mazishi ya kihistoria na yaliyofanyika kwa adhama kubwa nchini Lebanon ya mwanajihadi mkubwa na Katibu Mkuu shujaa na mpendwa wa Hizbullah Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah na Shahidi Sayyid Hashim Safiyyuddin huko nchini Lebanon, yalikuwa dhihirisho la umoja na mshikamano wa Muqawama na kuongezeka nguvu za Hizbullah ndani ya Lebanon, na kielelezo cha uungaji mkono madhubuti wa wananchi kwa harakati hiyo.
Qalibaf ameongeza kuwa: "Shahidi Nasrullah aling'ara mithili ya jua liangazalo juu ya mabega ya umati mkubwa wa wenye mapenzi ya dhati na yeye na kuwafikishia ujumbe walimwengu wa kwamba, kusimama imara kukabiliana na dhulma, uvamizi na jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni ni njia ya fikra; na njia ya fikra haiwezi kufutwa kwa jinai na mauaji".
Spika wa Bunge la Iran ameendelea kueleza: "katika ardhi azizi ya Lebanon, niliona wanaume na wanawake walio ngangari na imara, ambao walimpenda kwa ujudi wao wote kiongozi wao mpenzi na aliyewatoka wa Hizbullah; na kwa maana halisi ya maneno haya, na bila ya kutia chumvi, hawakuwa na woga wowote kwa adui na hawakuonyesha kuwa na chembe ya shaka au huzuni itokanayo na kukata tamaa ndani ya mioyo yao, bali walikuwa na imani ya dhati na ya ikhlasi juu ya Uislamu, njia ya fikra ya Imam Hussein AS na Bibi Zainab SA na malengo matukufu ya Muqawama".
Qalibaf ameongezea kwa kusema: "wakati jana nilipouona umati ule ulio thabiti huko Lebanon, ambao umesimama imara mithili ya mlima, niliifikia yakini kwa mara nyingine tena kwamba hakuna kafiri au mtenda jinai yeyote anayeweza kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu na kwamba hatimaye ukweli utajidhihirisha tu". Katika hotuba yake hiyo, Spika wa Bunge la Iran amebainisha kuwa: "katika uga wa kisiasa pia kutokana na jinsi Hizbullah ilivyoonyesha nguvu na uwezo wake, imemdhihirikia wazi kila mtu kwamba maadui hawawezi kuuondoa Muqawama au kuuweka kando ya ulingo wa kisiasa na kiusalama wa Lebanon kutokana na uungaji mkono wa wananchi ilionao. Hizbullah ni sehemu ya nguvu ya kitaifa ya Lebanon na mdhamini wa usalama na umoja uliokamilika wa ardhi yote ya nchi hiyo.../
342/
