4 Machi 2025 - 23:25
Source: Parstoday
Misaada ya kijeshi na silaha ambayo haijawahi kutolewa mfano wake ya serikali ya Trump kwa utawala wa Kizayuni wa Israel

Sambamba na Marekani kukata misaada yake kwa Ukraine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, siku ya Jumapili alitumia mamlaka ya dharura aliyonayo kisheria kupitisha mpango wa utoaji msaada wa shehena ya silaha zenye thamani ya dola bilioni 4 kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa hatua yake hiyo, serikali ya Trump itakuwa imetoa msaada wa silaha zenye thamani ya dola bilioni 12 kwa Israel katika muda wa siku 40 tu tangu ilipoingia madarakani, ikiwa ni sawa na kuupatia utawala huo wa Kizayuni msaada wa dola milioni 300 kwa siku.

Wizara ya ulinzi ya Marekani (Pentagon) nayo pia imetangaza kuwa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imeafiki kuiuzia Israel mabomu, zana za uteketezaji na silaha nyinginezo zenye thamani ya karibu dola bilioni tatu. Serikali ya Trump imetumia mamlaka ya dharura na kulitaarifu bunge yaani Kongresi kuhusu uwezekano wa kufanyika mauzo hayo, na kuweka kando taratibu za urasimu unaochukua muda mrefu, ambazo zingewapa fursa wenyeviti na wajumbe wa Kamati za Uhusiano wa Nje za Baraza la Wawakilishi na Seneti ya kuchunguza kwanza mauzo hayo.

Katika taarifa yake, Rubio amebainisha kuwa, serikali ya Trump, ambayo iliingia madarakani Januari 20, imeidhinisha mauzo ya silaha zenye thamani ya karibu dola bilioni 12 kwa utawala wa Kizayuni wa Israel; na akasisitiza kwamba Washington itaendelea kutumia nyenzo zote zilizopo kutimiza ahadi ya tangu na tangu iliyojifunga nayo Marekani ya kudhamini usalama wa Israel, ikiwa ni pamoja na nyenzo za kukabiliana na vitisho vya kiusalama. Aidha, amesisitiza kuwa ametumia mamlaka ya dharura aliyonayo kuharakisha ufikishaji wa misaada ya kijeshi kwa Israel ambayo ni mshirika wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, na ambayo sasa hivi iko kwenye utekelezaji wa makubaliano tete ya usitishaji vita iliyofikia na Hamas huko Ghaza. Hii ni mara ya pili katika kipindi cha wiki moja iliyopita kwa serikali ya Trump kutangaza hali ya dharura kwa ajili ya kuidhinisha kwa haraka mauzo ya silaha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tangu siku za mwanzoni mwa muhula wake wa pili wa urais, Donald Trump alianzisha tena mtindo aliokuwa akiutumia katika muhula wake wa kwanza wa kutoa uungaji mkono mkubwa na usio na mfano kwa utawala wa Kizayuni; na hatua mpya za hivi sasa ilizochukua serikali yake zimekuwa na muelekeo huohuo wa kuiunga mkono Israel na kuwapiga vita Wapalestina.

Hatua na misimamo hiyo imepokelewa kwa furaha na kwa mikono miwili na Tel Aviv. Hatua hizo ni pamoja na kutuma msaada mpya wa kijeshi kwa utawala wa Kizayuni na kupendekeza mpango wa kuwatimua wakazi wa Ghaza kwa kisingizio cha kulijenga upya eneo hilo kufuatia vita vya kinyama vya miezi 15 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni.

Gazeti la Wall Street Journal liliandika huko nyuma kuhusiana na suala hilo: “kwa kuzingatia vifo vya zaidi ya watu 46,600 huko Ghaza tangu vilipoanza vita katika Ukanda huo, Biden aliamua kufuta mauzo ya mabomu ya paundi 2,000 kwa Israel. Lakini mara baada ya Trump kuingia madarakani alibatilisha uamuzi huo; na katika kutetea na kuhalalisha hatua yake hiyo mbele ya waandishi wa habari, alisema: "Walishalipia na wamengojea kwa muda mrefu". Na kwa hatua yake hiyo, Trump akatoa kibali cha kuupatia utawala wa Kizayuni mabomu 1,800 hatari na yenye uzito kila moja wa paundi 2,000.

Itakumbukwa kuwa, katika muhula wake wa kwanza wa urais, kuanzia Januari 2017 hadi Januari 2021, Donald Trump alichukua misimamo na kupitisha maamuzi ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwa manufaa na maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ukweli ni kwamba, moja ya vielelezo vya wazi vya sera za nje za Trump ni msimamo wake wa kuuunga mkono bila masharti wala mipaka yoyote utawala haramu wa Israel na kutekeleza hatua ambazo marais wote waliopita wa Marekani hawakuwahi kuzichukua. Muhimu zaidi kati ya hatua hizo ni kuitambua Quds Tukufu (Jerusalem yote) kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni, kuitambua rasmi na kuihalalisha hatua ya Israel ya kupora Miinuko ya Golan ya Syria, kupendekeza mpango wa kikoloni wa Muamala wa Karne, ambao unaunufaisha na kuupa maslahi na upendeleo usio na kifani utawala wa Kizayuni sambamba na kuwanyima kikamilifu haki zao Wapalestina; na mwisho kabisa ni kuupa ridhaa utawala huo ghasibu ya kupora sehemu moja ya Ukingo wa Magharibi na kuiunganisha na maeneo mengine ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu yaliyopachikwa jina bandia la Israel.

Hatua aliyochukua sasa hivi Trump ya kuupa baraka kamili mpango wa kuupatia mabomu ya paundi 2,000 utawala wa Kizayuni wa Israel na kuchukua msimamo kwa maafikiano na Tel Aviv wa kuwafukuza Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza, inafuata mwelekeo uleule aliochukua wakati wa muhula wake wa kwanza wa urais wa kuutumikia utawala ghasibu wa Israel.

Kwa hiyo kuupatia utawala wa Kizayuni misaada ya fedha na silaha yenye thamani ya dola bilioni 12 ndani ya muda wa siku 40 tu za muhula wa pili wa urais wa Donald Trump ni ishara ya muelekeo ambao serikali ya Trump imedhamiria kuufuata katika kipindi cha miaka minne ijayo kuhusiana na kuuunga mkono kwa kila hali utawala huo dhalimu…/

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha