Kundi la UK Screen Industry lilituma barua kwa wanachama wa Kamati ya Utamaduni, Vyombo vya Habari na Michezo (CMS) ya Bunge la Uingereza siku ya Jumatatu, wakiomba maelezo juu ya sababu za kuondolewa kwa filamu hiyo iliyopewa jina "Gaza: How to Survive a Warzone" kutoka kwa jukwaa la BBC iPlayer.
Barua hiyo ilitumwa siku moja kabla ya mkurugenzi mkuu wa BBC, Tim Davie, na mwenyekiti wake, Dr. Samir Shah, kufikishwa mbele ya kamati hiyo kwa mahojiano.
Filamu hiyo, iliyotangazwa kwa mara ya kwanza tarehe 17 Februari, inahusu maisha ya kijana wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 14 aitwaye Abdullah al-Yazouri.
BBC iliondoa filamu hiyo ya tukio la kweli kwa sababu baba yake Yazouri, Dkt. Ayman al-Yazouri, ni naibu waziri wa kilimo wa Gaza.
UK Screen Industry iliwataka wabunge wa Uingereza kumuuliza Davie na Dr. Shah waeleze viwango vya uhariri walivyotumia na mchakato wa uamuzi uliosababisha kuondolewa kwa filamu hiyo , hatua ambayo imezua wasiwasi wa ubaguzi wa rangi na ubanaji maudhui.
Kundi hilo pia limeitaka Kamati ya CMS kuuliza BBC jinsi inavyopanga kudumisha ahadi yake ya kutoegemea upande wowote na kulinda uhuru wa kujieleza katika maamuzi yake ya siku zijazo kuhusu vipindi vya habari.
Wamesema kuwa watu wengi sasa wanahisi BBC si mahali salama kwa watayarishi wa vipindi vinavyoangazia mateso ya Wapalestina.
Wiki iliyopita, kundi la waandishi wa habari na wataalamu wa vyombo vya habari wa Kiyahudi wapatao 45, akiwemo mkurugenzi wa zamani wa BBC, Ruth Deech, walishinikiza shirika hilo kwa kutuma barua wakisema filamu hiyo iondolewe kutoka jukwaa la BBC iPlayer, wakimuita waziri wa Gaza "kiongozi wa kigaidi".
Hadi sasa, watu 735 wametia saini kwenye barua inayoitaka BBC kusitisha kile wanachokiita "ubanaji habari kuhusu Palestina", wakionya kuwa hatua ya shirika hilo inaleta dosari katika maadili ya uandishi wa habari kwa kuweka mbele mashinikizo ya kisiasa badala ya maslahi ya umma.
Your Comment