5 Machi 2025 - 22:45
Source: Parstoday
Jaji wa Kijapani achaguliwa kuwa rais wa ICJ, atasimamia kesi ya mauaji ya kimbari ya Israel

Mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa imemchagua jaji wa Kijapani kuwa rais wake mpya, akichukua nafasi ya Nawaf Salam aliyeng’atuka madarakani Januari ili kuwa waziri mkuu wa Lebanon.

Katika taarifa, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imesema Jaji Yuji Iwasawa ataongoza mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague hadi Februari 5, 2027, wakati muhula wa Salam ulitarajiwa kumalizika.

Iwasawa alijiunga na ICJ Juni 2018. Kabla ya kujiunga na mahakama hiyo ya majaji 15, alikuwa profesa wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Tokyo na mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu.

Jaji huyo mwenye umri wa miaka 70 ni Mjapani wa pili kushika urais wa ICJ baada ya Hisashi Owada, ambaye alihudumu kama mkuu wa mahakama hiyo kati ya 2009 na 2012.

Salam, ambaye alianza jukumu lake kama mkuu wa ICJ mnamo Februari 2024, alijiuzulu rasmi baada ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu wa Lebanon na Rais Joseph Aoun.

Jaji Julia Sebutinde, mwenye msimamo wa kuupendelea utawala wa Israel na ambaye ni raia wa Uganda, alikuwa anashikilia urais wa muda wa mahakama hiyo.

ICJ kwa sasa inashughulikia kesi kadhaa kubwa, ikiwemo ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel.

Afrika Kusini iliwasilisha malalamiko mahakamani Desemba 2023, ikisema vitendo vya utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza ni “mauaji ya kimbari kwa sababu vinakusudia kuangamiza sehemu kubwa ya kundi la kitaifa, kabila na jamii ya Kipalestina.”

Tangu wakati huo, mataifa kadhaa, yakiwemo  ya Belize, Cuba, Nicaragua, Colombia, Libya, Mexico, Palestina, Uhispania, Uturuki, Bolivia, Maldives, Chile na Ireland, yamejiunga na kesi hiyo.

Mnamo Januari 2024, ICJ ilitoa uamuzi wa kuamuru Israel ichukue hatua zote zilizo ndani ya uwezo wake kuzuia mauaji ya kimbari huko Gaza, lakini haikutoa agizo la kusitisha mapigano mara moja.

Israel ilianzisha mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, lakini haikufanikisha malengo yake yaliyotangazwa licha ya kuwaua Wapalestina wasiopungua 48,397, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Utawala huo wa kikoloni wa Isarel ulikubali masharti ya mazungumzo ya muda mrefu yaliyowekwa na Harakati ya Muqawama ya Hamas chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, ambayo yalianza kutekelezwa Januari 19.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha