Mohsen Naziri-Asl, alitoa onyo na indhari hiyo siku ya Jumatano (Machi 5) katika kikao cha Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA mjini Vienna na akabainisha: "Troika ya Ulaya haiko katika nafasi ya kisheria au ya kimaadili ya kuamilisha utaratibu wa mzozo dhidi ya Iran, kwa sababu Troika hiyo imekiuka Azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na JCPOA".
Naziri-Asl aliashiria jinsi Iran inavyoheshimu misingi ya kuzuia uenezaji silaha za nyuklia na makubaliano yaliyopo baina yake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuhusiana na suala hilo na akaongezea kwa kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuzingatia misingi yake yenye nguvu ya kiitikadi na kistratejia inazichukulia silaha za maangamizi ya umati na hasa silaha za nyuklia kuwa ni kitu kilichopitwa na wakati, si cha kiutu na chenye madhara kwa amani na usalama wa kimataifa".
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ofisi ya Umoja wa Mataifa amekosoa pia upande wa pili iliofikia makubaliano nao kwa kutotimiza wajibu wake, wakati Iran imeshikamana kikamilifu na majukumu yake kulingana na makubaliano hayo na akasema: "kwa kupitia 'kurejesha katika hali ya kawaida miamala ya kibiashara na kiuchumi na Iran', JCPOA ilitakiwa ikidhi maslahi ya wote, lakini je, natija hiyo imepatikana? Tangu mwanzoni kabisa, na hata kabla ya kujitoa, Marekani, ilidhamiria kwa nia mbaya kuzuia kurejeshwa katika hali ya kawaida uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na Iran na kuinyima manufaa ya kiuchumi yaliyoainishwa katika JCPOA.
Katika kutekeleza sera zake zenye misingi mikuu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitahadharisha kila mara kuhusu namna Marekani na upande wa Ulaya zinavyokhalifu na kutotekeleza ahadi na majukumu yao kuhusiana na JCPOA na maazimio ya Umoja wa Mataifa. Maafisa wa Iran wamechukua hatua na misimamo kulingana na namna upande wa pili unavyokhalifu ahadi zake.
Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani na pande za Magharibi zimetumia kila fursa kueneza hujuma na propaganda hasi za vyombo vya habari dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran, wakati utawala haramu wa Kizayuni unaongeza maghala yake ya nyuklia kwa kuungwa mkono na kufumbiwa macho na Marekani na serikali za Magharibi, hatua ambayo itakuwa ni tishio kubwa kwa usalama wa kikanda na itavuruga zaidi utulivu na uthabiti.
Kinyume na madai na uwongo wa Magharibi, ni muelekeo huo wa undumakuwili uliofuatwa na Marekani na Magharibi katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ndio sababu kuu ya kukosekana utulivu katika eneo. Serikali za Washington na Ulaya sambamba na kuuunga mkono kikamilifu utawala wa Kizayuni, zimenyamazia kimya mipango yake ya kijeshi na kuuzatiti kwa silaha za maangamizi ya umati.
Kwa miaka kadhaa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitekeleza kikamilifu ahadi na majukumu yake ya nyuklia na kupunguza shughuli zake, uzalishaji na ufanyaji kazi wa vituo vyake, lakini katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Trump, mnamo mwezi Mei 2018, Marekani ilijitoa katika mapatano ya JCPOA na kutekeleza vikwazo vikali zaidi dhidi ya Iran kupitia sera ya mashinikizo ya juu kabisa.
Kwa upande mwingine, kwa kuzingatia ukiukaji wa mara kwa mara wa kutekeleza ahadi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya katika kundi la 4+1, Tehran ilipunguza kwanza kutekeleza ahadi zake za nyuklia katika hatua tano na kisha ikachukua hatua mpya ya kustawisha shughuli zake za nyuklia nje ya mipaka ya JCPOA kwa kutekeleza azimio la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani Bunge la Iran.
Kwa mujibu wa vifungu vya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, vikwazo na vizuizi ilivyowekewa Iran vilimalizika tarehe 18 Oktoba 2023, miaka 8 baada ya JCPOA. Hata hivyo, Marekani na Troika ya Ulaya hadi sasa hazijatimiza wajibu wao, kinyume na ilivyoainishwa kwenye vifungu vya azimio hilo.
Katika mazingira hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetumia uwezo wake wa ndani na juhudi, hima na uwezo wa vijana wake wataalamu wa Kiirani na kufanikiwa kustawisha sekta yake ya nyuklia licha ya vikwazo na vizuizi vyote ilivyowekewa. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitangaza kila mara kuwa malengo haramu na ya kisiasa ya Marekani na washirika wake wa Ulaya yatakabiliwa na majibu na hatua za kujibu mapigo za Iran.
Troika ya Ulaya, nayo pia licha ya kutoa ahadi nyingi baada ya Marekani kujiondoa katika JCPOA, sio tu imeshindwa kutekeleza majukumu yake ya kuondoa vikwazo, bali pia imekuwa mshirika wa Marekani katika kushadidisha mashinikizo dhidi ya Iran; na hii ni ishara ya kuendelea nchi za Ulaya kukhalifu ahadi zao.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tehran imetumia vyema hatua za kidiplomasia kufanikisha sera zake za nje; na katika kukabiliana na mipango miovu na hatua haribifu za Marekani na Troika ya Ulaya, imeubainishia ulimwengu kupitia vikao vya Umoja wa Mataifa malengo na madhumuni yake ya kutumia na kustawisha sekta yake ya nyuklia.../
342/
Your Comment