13 Machi 2025 - 17:27
Source: Parstoday
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi: Wito wa Trump wa kufanya mazungumzo na Iran ni 'ulaghai' tu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, wito wa Rais Donald Trump wa Marekani kwamba anataka kufanya mazungumzo na Iran si lolote bali ni jaribio la "kuhadaa maoni ya umma duniani" na kutaka kuonyesha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ni upande ambao hauko tayari kutoa fursa nyingine kwa diplomasia.

Ayatullah Khamenei aliyasema hayo jana alipohutubia hadhara ya wanachuo hapa mjini Tehran na akabainisha: "tulikaa kitako kwa miaka kadhaa na kujadiliana. Mtu huyuhuyu aliitupilia mbali meza na kurarua (hati za) mazungumzo yaliyohitimishwa, yaliyokamilishwa na yaliyotiwa saini".

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amehoji: "wakati tunajua kwamba yeye haheshimu [makubaliano], kuna maana gani ya kufanya mazungumzo? Kwa hivyo, wito wa mazungumzo na wa kuzungumza ili kujadiliana unalenga kuhadaa maoni ya umma duniani".

Ayatullah Khamenei amesema, utawala wa Trump hauna nia ya kuondoa vikwazo hivyo, na kwamba mazungumzo yatayafanya mashinikizo yawe mabaya zaidi kwa sababu Washington itaibua matakwa mengine mapya.

"Ikiwa madhumuni ya mazungumzo ni kuondoa vikwazo, mazungumzo na utawala huu wa Marekani hayataondoa vikwazo. Yatavifanya vikwazo viwe vikali zaidi na kuongeza mashinikizo”, amebainisha Kiongozi wa Mapinduzi. 

Akijibu madai ya nchi za Magharibi kwamba Iran inataka kuunda silaha za nyuklia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwa mara nyingine tena kuwa Iran haitaki kutengeneza silaha za nyuklia na akaongeza kuwa, kama ingechagua kufanya hivyo, sasa hivi ingekuwa tayari imeshaunda.

“Inasemwa kwamba ‘hatutairuhusu Iran ipate silaha za nyuklia.’ Kama tungetaka kutengeneza silaha za nyuklia, Marekani isingeweza kutuzuia. Ukweli wa kwamba hatuna silaha za nyuklia na hatufuatilii kuwa nazo ni kwa sababu sisi wenyewe hatuzitaki kwa sababu maalumu", ameeleza bayana Ayatullah Khamenei.

Akizungumzia vitisho vya Marekani vya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonya kwamba Iran imeshajiandaa kutoa jibu kali, na akaongeza kuwa Marekani ndiyo itakayoumia zaidi katika makabiliano hayo.

“Kwa maoni yangu, kitisho hiki hakina mantiki kwa sababu vita au uvamizi wa kijeshi si suala la upande mmoja. Iran ina uwezo wa kujibu mapigo, na bila shaka itakapolazimu itafanya mashambulio ya kujibu shambulio. Na hata ninaamini kwamba ikiwa Wamarekani au mawakala wao watafanya kosa la kuchukua hatua watapata hasara zaidi kuliko mtu mwingine yeyote", amesema Ayatullah Khamenei.

Kuhusu suala la vikwazo, amebainisha kuwa, hatua hizo zinapoteza athari zake hatua kwa hatua kwa sababu Iran imeshapata njia za kuvizima.

Kiongozi wa Mapinduzi amesema: "baada ya kupita muda, wakati vikwazo vinapoendelezwa ulimwenguni kote, polepole hupoteza athari zake. Hata wao (maafisa wa Marekani) wenyewe wanalikiri hili. Wanakubali kwamba nchi inayowekewa vikwazo inaweza hatua kwa hatua kutafuta njia za kuzima athari za vikwazo na kuvifanya visiwe na taathira. Tumegundua njia nyingi kama hizo na tumezima athari za vikwazo katika maeneo mengi”.

Pamoja na hayo, Ayatullah Khamenei amesema, changamoto nyingi za kiuchumi za Iran zinatokana na uzembe wa ndani na uendeshaji mbovu kuliko vikwazo vya nje.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha