15 Machi 2025 - 21:53
Source: Parstoday
Associated: Marekani na Israel zilitaka kuwapa makazi wakazi wa Gaza katika nchi tatu za Kiafrika

Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa Marekani na Israel zilitoa pendekezo kwa maafisa wa nchi tatu za Afrika la kuwapa makazi Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza kwenye ardhi za nchi hizo.

Shirika hilo limewanukuu maafisa wa Marekani na Israel wakisema kuwa, Washington na Tel Aviv zimewasiliana na maafisa katika nchi tatu za Afrika Mashariki kujadili suala la kutumia maeneo ya nchi hizo kuwapa makazi Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza.

Associated Press imenukuu duru hizo zikisema kuwa, mawasiliano yamefanywa na maafisa kutoka Sudan, Somalia, na eneo lililojitenga la Somaliland kuhusiana na pendekezo hilo.

Shirika hilo liliongeza kuwa maafisa wa serikali ya Sudan wamesema walikataa pendekezo hilo la Marekani, huku maafisa kutoka Somalia na Somaliland wakikana kuwepo mawasiliano ya aina yoyote kuhusiana na suala hili.

Maafisa wawili wa Sudan, wakizungumza na shirika hilo kwa sharti la kutotajwa majina, wamethibitisha kuwa utawala wa Donald Trump umewasiliana na serikali ya Sudan kuhusu suala la kuwapa Wapalestina kutoka Gaza makazi mapya nchini Sudan, lakini Khartoum imekataa mara moja pendekezo hilo.

Mmoja wa maafisa hao amesema kwamba serikali ya Donald Trump iliahidi msaada wa kijeshi kwa serikali ya Sudan dhidi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), ujenzi mpya wa baada ya vita, na motisha zingine.

Shirika hilo limesema kuwa mawasiliano ya Marekani na Israel na nchi za Sudan, Somalia, na eneo lililojitenga na Somalia linalojulikana kama Somaliland yanaonyesha azma ya Washington na Tel Aviv ya kusonga mbele na mpango wa kuwaondoa Wapalestina eneo la Ukanda wa Gaza ambao umelaaniwa kimataifa na kuibua mjadala mzito wa kisheria na kimaadili.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha