17 Machi 2025 - 18:24
Source: Parstoday
Hizbullah: Lebanon haitaanzisha katu uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni Israel

Mwakilishi wa Hizbullah katika Bunge la Lebanon amesisitizia msimamo wa kudumu wa nchi hiyo kuhusiana na utawala wa Kizayuni wa Israel na akasema, Lebanon kamwe haitokubali kufuata mkondo wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo ghasibu.

Ali Fayyad, ambaye ni mbunge wa mrengo wa Uaminifu kwa Muqawama katika Bunge la Lebanon ameyasema hayo alipohutubia hafla iliyofanyika katika eneo la Jabal Amel kwa mnasaba wa kuadhimisha Siku ya Mwalimu na mwezi mtukufu wa Ramadhani kwamba Lebanon haitawahi kamwe na katika hali yoyote ile, kuelekea kwenye mkondo wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel.

Fayyad ameuelezea utawala wa Kizayuni kuwa ni adui mwenye mgongano na ujudi, utambulisho na maslahi ya Lebanon, na akaonya pia kwa kusema: "yasifanyike makosa katika ufanyaji mahesabu kuhusiana na Muqawama, kwa sababu msimamo wetu umejengeka juu ya msingi wa kuzikomboa kikamilifu ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kulinda mamlaka ya kujitawala ya Lebanon dhidi ya ubeberu wa Marekani na utawala wa Kizayuni.

Mbunge huyo wa Lebanon ameielezea hali ya nchi hiyo kuwa ni mbaya sana na akasema, licha ya kuwepo matumaini ya kuboreka hali ya mambo, kuendelea uchokozi unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel, kukaliwa kwa mabavu baadhi ya maeneo ya ardhi ya Lebanon, kupuuzwa na utawala huo wa Kizayuni vipengee vya azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mashinikizo yanayotolewa na Marekani ambayo yanafanyika kwa uratibu na hatua za Tel Aviv, ni kizuizi kikubwa kwa machakato huo.

Fayyad ametoa matamshi hayo baada ya chombo cha habari cha Marekani cha Axios kuripoti siku ya Jumanne (Machi 11) kwa kuwanukuu maafisa wawili wa Washington wakieleza kwamba Israel na Lebanon zimekubali kuanza mazungumzo ya kutatua tofauti zao za muda mrefu kuhusu mpaka wa ardhini.

Utawala wa Kizayuni umepuuza muda ulioainishwa wa kuondoa vikosi vya jeshi lake kusini mwa Lebanon na unaendelea kukalia kwa mabavu maeneo kadhaa ya ardhi ya nchi hiyo.

Hatua hiyo ya Tel Aviv inajiri huku utawala huo ghasibu ukikiuka mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano na kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya maeneo ya mpakani mwa Lebanon.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha