20 Machi 2025 - 17:32
Source: Parstoday
Mkesha wa kwanza wa Laylatul Qadr waadhimishwa Iran na maeneo mengine duniani

Usiku wa kuamkia leo Alkhamisi yaani mwezi 19 Ramadhani, ulikuwa ni mkesha wa kwanza wa Laylatul Qadr na umeadhimishwa katika kona zote za Iran na maeneo mengine duniani.

Alfajiri ya mwezi 19 ya Ramadhani, Abdur Rahman bin Muljim al Muradi, mwanachama wa kundi la Khawarij, alimshambulia kwa upanga wenye sumu Imam Ali (AS) ndani ya Mihrabu, wakati walipokuwa anasalisha Sala ya Alfajiri. Imam Ali alilazwa nyumbani kwake baada ya kupigwa upanga huo na aliuawa shahidi siku mbili baadaye, yaani mwezi 21 Ramadhani.

Imam Ali bin Abi Talib AS ni shakhsia wa pili baada ya Mtume Muhammad SAW ambaye anaelezwa na historia ya Uislamu kwamba alikuwa shujaa, Simba wa Mungu aliyekuwa akishinda kwenye vita vyote, mtu aliyekuwa na imani thabiti, halisi, akhlaki njema, ilmu na uadilifu wa kupigiwa mfano. Alipata ilmu na malezi bora kabisa kutoka kwa Mtume Muhammad mwenyewe SAW akiwa bado mtoto mdogo.

Nyusiku za 19, 21, na 23 za Ramadhani ni mikesha ya Laylatul Qadr hasa kwa Waislamu wa madhehebu ya Kishia na ndani yake Waislamu hukesha usiku kucha Misikitini kusoma Quran, kusali, kuomba dua na kufanya ibada nyinginezo. Laylatul-Qadr ni usiku wenye cheo ambao Qur'ani Tukufu inasema ni bora kuliko miezi elfu moja. 

Mbali na Waislamu wa Iran, mkesha wa jana usiku wa Laylatul Qadr uliadhimishwa pia katika nchi nyingine za Afrika, Ulaya, Asia na Amerika ambapo maashiki wa Ahlul Baytu wa Mtume Muhammad SAW walijumuika pamoja kwa ibada na kukumbuka siku Imam Ali AS alipopigwa upanga wenye sumu.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha