Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni amesisitiza kuwa, vikosi vya utawala huo wa kibaguzi vitashambulia wakazi wa ukanda huo kwa nguvu maradufu, na kuwa kuanzia sasa hakuna mazungumzo yatakayofanyika isipokuwa "chini ya moto".
Israel imefanya mashambulizi zaidi ya 200 ya anga huko Gaza tangu Jumanne asubuhi, na kusababisha zaidi ya watu 416 kuuawa shahidi, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, wakiwemo watoto 170. Baada ya gharama kubwa ya kibinadamu ambayo Gaza ililipa siku ya Jumanne, jeshi la Israel lilianzisha tena mashambulizi yake kwenye eneo hilo siku ya Jumatano kwa kulenga maeneo 20 tofauti huko Gaza na pia kuonya tena kuhusu uhamishaji wa lazima dhidi ya wakazi wa maeneo kadhaa mashariki mwa Gaza. Aidha, Jeshi la Wanamaji la Israel limeshambulia boti kadhaa za chama cha Jihad Islami katika pwani ya Gaza. Wakati huo huo, shirika la habari la Quds lenye mafungamano na Hamas limesema kuwa, idadi ya mashahidi wa mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel imefikia watu 429.
Katika mashambulizi mapya ya Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza, hakuna eneo lolote lililosalimika na mashambulizi, ambapo utawala wa Kizayuni umekuwa ukilenga kwa makusudi nyumba za makazi, shule, vituo vya wakimbizi na mahema wanamoishi. Israel inadai kuwa imeanzisha mashambulizi hayo mapya baada ya Hamas kukataa kuongeza muda wa usitishaji mapigano na kuwaachilia mateka zaidi. Tangu kumalizika hatua ya kwanza ya usitishaji vita wiki mbili zilizopita, pande mbili hazijaweza kufikia makubaliano kuhusu awamu ya pili ya mazungumzo hayo, ambayo ni pamoja na kuachiliwa mateka waliosalia wa Kizayuni, kumalizika vita na kuondolewa kikamilifu majeshi ya Israel huko Gaza. Katika upande mwingine utawala wa Kizayuni unasisitiza kuwa, utaendeleza vita hadi kuangamizwa kabisa uwezo wa kijeshi na kiserikali wa Hamas na kuachiliwa huru mateka wote wa Kizayuni.
Katika siku za hivi karibuni, Netanyahu amekutana na viongozi wengine wa utawala wa Kizayuni na akachagua moja ya machaguo yaliyopendekezwa na jeshi la utawala huo. Chaguo hili linajumuisha kufanya mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya makumi ya maeneo ya Gaza, ikiwa ni pamoja na kuwaua makamanda wa kati na waandamizi wa Hamas ambao wamekuwa wakifanya harakati za kuhuisha nguvu ya kundi hilo, lakini si viongozi wake wa ngazi za juu, kama ripoti zinaonyesha kuwa maafisa 5 wa Hamas tayari wameuawa shahidi.
Nukta muhimu ni kwamba, mashambulizi makubwa ya anga na makombora ya utawala wa Kizayuni yanafanyika kwa uelewa kamili na ruhusa ya Marekani. Ikulu ya White House imetangaza kuwa Israel ilishauriana na utawala wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo kabla ya kushambulia Gaza. Ni muhimu kukumbuka kwamba Trump, ambaye ana historia ndefu ya uungaji mkono wa pande zote kwa Israel, alitoa mara mbili amri ya kuachiliwa huru mateka wote wa Kizayuni na kuitishia Hamas kuwa itaangamizwa kabisa iwapo amri hiyo haitatekelezwa.
Kuna maoni mbalimbali yanayotolewa kuhusu malengo ya Benjamin Netanyahu katika kuanzisha mashambulizi mapya huko Gaza. Gazeti la Washington Post limefichua kwamba kuanza tena kwa vita vya Gaza kimsingi ni "mbinu ya mazungumzo" inayotumika kwa ajili ya kuishinikiza Hamas ipunguze matakwa yake baada ya wiki kadhaa za mazungumzo magumu. Inaonekana kwamba lengo kuu la utawala wa Kizayuni ni kutoa mashinikizo kwa Hamas ili iwaachilie huru mateka waliosalia wa Kizayuni, ambao Netanyahu anadai kuwa ni zaidi ya watu 60, katika fremu ya awamu ya kwanza ya usitishaji vita, bila ya utawala huo kutaka kufikia awamu ya pili ya usitishaji vita. Kwa njia hii, na kwa mtazamo wa viongozi wa utawala wa Kizayuni, Hamas na makundi mengine ya muqawama wa Palestina hayatakuwa na turufu yoyote katika awamu ya pili ya usitishaji vita, ambapo Tel Aviv inaweza kushiriki katika mazungumzo ya baadaye ikiwa na nafasi ya juu na kufanya chochote inachotaka dhidi ya wakazi wa Gaza na makundi ya muqawama.
Wakati Israel inasisitiza kwamba hakuna mazungumzo yatakayofanyika isipokuwa chini ya moto wa vita, Hamas kwa mara nyingine imesema kuwa haijafunga mlango wa mazungumzo na hakuna haja ya makubaliano mapya, kwa sababu makubaliano ambayo yameidhinishwa na pande zote bado ni halali na yanapaswa kutekelezwa. Imewataka wapatanishi na jamii ya kimataifa kuilazimisha Israel ikomeshe uvamizi, itekeleze makubaliano ya kusitisha vita na kuwezesha kuanza awamu ya pili ya makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa tarehe 19 Januari.
Osama Hamdan, mjumbe wa ngazi ya juu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina (Hamas) pia amesema katika taarifa kwamba, juhudi zote za mjumbe maalum wa Marekani Steve Whitkoff ni kuhitimisha makubaliano ya awali na kufanya mapatano mapya na utawala wa Kizayuni.
Misri siku ya Jumanne iliwasilisha pendekezo jipya la kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza, ambalo linachukuliwa kama daraja la kusuluhisha tofauti zilizopo na kuwasilisha njia ya kati kwa kati ya pendekezo lililokubaliwa hapo awali na Hamas, ambalo ni pamoja na kuachiliwa Alexander Eidan, mwanajeshi mwenye uraia wa Marekani na Israel, na miili ya wafungwa watano, na pendekezo lililotolewa na Marekani kwa ajili ya kuachiliwa nusu ya wafungwa walio hai na miili ya wale walioaga dunia. Pendekezo hili ni pamoja na kusitishwa mapigano, kufunguliwa tena kivuko cha Rafah na kuruhusiwa misaada ya kibinadamu iingie Gaza na kuachiliwa idadi kubwa ya mateka wa Israel waliojeruhiwa na miili ya wafungwa wenye uraia wa mataifa mawili. Jana Hamas ilisisitiza kuwa imelegeza kidogo misimammo yake katika mazungumzo na kukubaliana na pendekezo la Steve Wittkoff, mwakilishi maalum wa rais wa Marekani.
Kwa maelezo hayo tunaweza kusema kuwa, Washington na Tel Aviv zimeshirikiana katika kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya watu adhulumu wa Ghaza kwa visingizio mbalimbali, na kwa hakika mjumbe huyo maalum wa Marekani kwa kutangaza mpango mpya amevuruga mchakato wa utekelezaji wa awamu ya pili ya usitishaji vita na kuandaa mazingira yanayohitajika kwa ajili ya kuanza tena mashambulizi ya Israel huko Gaza.
342/
Your Comment