22 Machi 2025 - 04:30
Ramadhan ni Mwezi ambao dhambi zote zinaunguzwa (zinafutwa) ndani yake

Mja asikose wala asikate tamaa katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, bali akithirishe kwa wingi kuomba sana maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu, kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, na anasamehe dhambi za aina yoyote ile (ispokuwa dhambi ya kumshirikisha).

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-; Sheikh Dk. Alhad Mussa Salum al-Naqshbandi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), katika darsa lake juu ya umuhimu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kupitia Televisheni ya IBN TV AFRIKA, amefafanua na kubainisha maana ya neno Ramadhan ambalo ndilo jina la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kwamba ni kwa nini Mwezi huu umeitwa kwa jina hilo. Akifafanua na kubainisha somo hilo amesema kama ifuatavyo:

Mwenyezi Mungu ametuwekea Mwezi huu sisi Ummah wa Muhammad (s.a.w.w) ili aweze kutusamehe dhambi zetu na makosa yetu. Na hii ndio maana ya jina lenyewe "Ramadhani", linalomaanisha kuwa Mwenyezi Mungu anawasamehe na kuwafutia waja Wake dhambi zao.

Kwa mantiki hiyo; Mja asikose wala asikate tamaa katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, bali akithirishe kwa wingi kuomba sana maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu, kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, na anasamehe dhambi za aina yoyote ile (ispokuwa dhambi ya kumshirikisha)... na hivi ndivyo Allah (swt) alivyobainisha ndani ya Kitabu chake Kitukufu aliposema:

"قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنْفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِنْ رَحْمَةِ اللَّهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ"


"Sema enyi waja wangu waliozifanyia israfu nafsi zao! Msikate tamaa na rehma za Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwingi wa Maghfira, Mwenye Kurehemu". (Surat Zumar: Aya 53).

Hivyo Allah (s.w.t) anasemehe dhambi zote za mja Wake; ispokuwa dhambi ya shirki (kumfanyia mshirika Mwenyezi Mungu); kama alivyosema (s.w.t) katika Aya hii Tukufu:


"إِنَّ اللَّهَ لَا يَغْفِرُ أَنْ يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَنْ يَشَاءُ ۚ وَمَنْ يُشْرِكْ بِاللَّهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا"


"Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kufanyiwa mshirika, lakini husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye. Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu hakika amezusha dhambi kubwa".(Surat Al-Nisaa: Aya ya 48).

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atusamehe sote dhambi zetu na makosa yetu, na atuepushe na dhambi kubwa ya kumshirikisha isiyosameheka.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha