Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-; Sheikh Said Othman, Mtafiti na Mchambuzi wa Masuala ya Kiislamu, na ambaye piani Sheikh wa Mkoa wa Dar-es-Salam chini ya Mwavuli wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania (T.I.C), akiwa katika kipindi cha Uislamu na Jamii | Kipindi cha Maswali na Majibu, kupitia Televisheni ya IBN TV AFRIKA, amesema: Imam Ali (a.s), katika sifa nzuri zilizodhihiri sana kwake, ni ushujaa wake. Waislamu wote wanalijua hili. Wakisikia Jina la Ali linatajwa, moja kwa moja kinachotangulia katika ubongo wao ni sifa ya Ushujaa wa Ali (a.s). Hakika yeye alikuwa ni Shujaa sana na jasiri kuliko Masahaba wote. Yeye ni Shujaa wa Uislamu na Waislamu. Na ushujaa siku zote unaendana na nguvu ya Imani na nguvu ya mwili vile vile.
Na ukiwa Muumini imara na Shujaa, wewe bora kuliko Muumini dhaifu. Na hivi ndivyo alivyosema Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) katika Hadithi isemayo:
"المُؤْمِنُ الْقَوِيُّ خَيْرٌ وأَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنَ الْمُؤْمِنِ الضَّعِيفِ".
"Muumini mwenye nguvu (Shujaa na Jasiri) ni bora na mwenye kupenda zaidi na Mwenyezi Mungu kuliko Muumini dhaifu".
Kwa hiyo, Imam Ali (a.s) alikusanya:
1-Imani ya hali ya juu.
2- Na vile vile nguvu ya mwili.
Mambo haya mawili ndiyo yaliyofanya Imam Ali (a.s) kuwwa Shujaa na Jasiri, mpaka akepewa Lakabu ya:
(أسد الله الغالب )
"Simba wa Mwenyezi Mungu mwenye kushinda"
Hii ni Lakabu ya kipekee ya Amirul Muuminina Ali bin Abi Talib (a.s).
Na sababu ya Imani ya Imam Ali (a.s) kuwa ya daraja ya juu na yenye mizizi imara na uthabiti, ni hii kwamba yeye amelelewa katika Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), na Mlezi wake na Mwalimu wake ni mwenyewe Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Kwa hiyo, Imam Ali (a.s) anakumbukwa na Ulimwengu wote wa Kiislamu kuwa yeye ni Shujaa wa Kiislamu, aliyeupigania Uislamu, na kuuhami Uislamu kwa ushujaa wake na ujasiri wake, daima aliutetea uhai wa Uislamu na aliuheshimisha Uislamu kupitia Upanga wake, kama ambavyo Ummul - Muuminina Khadija (s.a) aliuhamia na kuuheshimisha Uislamu kupitia Mali yake. Na Uislamu huu umekuwa imara na thabini na hatimaye kutufikia hata sisi tunaoishi katika zama zetu za leo hii kutokana na vitu hivi viwili: Upanga wa Ali bin Abi Talib (a.s) na Mali ya Mama yetu, Sayyidat Khadija (s.a), ambaye ni Mke Kipenzi wa Bwana wetu Mtume Muhammad (s.a.w.w), ambapo siku zote alijivunia kuwa na Mke kama Sayyidat Khadija (s.a).
Kumpenda Ali bin Abi Talib (a.s) ni Wajibu
Lakini kubwa zaidi ambalo ni lazima kwa kila Muislamu kulijua na kulifanya, ni hili kwamba:
Ali bin Abi Talib (a.s) ni katika watu ambao ni wajibu kwa kila Muislamu kuwapenda. Kwa maana kwamba Ali (a.s) kumpenda sio suala la kujisikia kuwa unaamuaje, bali ni suala la wajibu kumpenda, na sio hiari.
Ali (a.s) ni katika watu ambao wanadamu/ waja wa Allah (swt) wanatakiwa kuhakikisha anaenea katika nyoyo zao, na hilo ni kwa mujibu wa Qur'an Tukufu pindi Allah (swt) alipomwambia Mtume (saww) atwambie sisi waja Wake namna hii:
"قُلْ لَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِلَّا الْمَوَدَّةَ فِي الْقُرْبَىٰ"
"Sema: Kwa haya siombi malipo yoyote kwenu ispokuwa mapenzi ya kuwapenda watu wangu wa karibu (Ahlul-Bayt a.s)". (Surat Ash-Shura: Aya ya 23).
Kwa mujibu wa Aya hii Tukufu, Imam Ali (a.s) ni katika watu Watano ambao ni lazima / ni wajibu kwetu kama Waislamu kuwapenda.
Si hilo tu, bali pia Imam Ali (a.s) ni katika watu ambao; tunaposwali swala yoyote ile, ni lazima kutawaja na kuwatakia amani katika swala zetu; lazima tuseme:
"اللهم صلي على محمد وآل محمد"
"Ewe Mwenyezi Mungu! Mswalie Muhammad na Aali zake Muhammad".
Na yeyote asiyewaswalia Ahlul-Bayt(a.s) wa Mtume Muhammad (s.a.w.w); huyo hana swala; Bali swala yake ni batili. Sasa huyu Amirul-Muuminina, Ali bin Abi Talib (a.s) ni katika hao watukufu na watoharifu ambao usipomswalia na kumtakia rehma katika swala yako, wewe swala huna. Na ukisema:
"اللهم صلي على محمد وآل محمد"
"Ewe Mwenyezi Mungu! Mswalie Muhammad na Aali zake Muhammad".
Basi jua na tambua kwamba Imam Ali (a.s) yumo ndani yake na tayari umemtakia rehma na amani katika swala yako (Kwa maana umemswalia).
Kwa hiyo, Imam Ali (a.s) ni Swahaba mkubwa na ni Swahaba Mwandamizi wa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w).
Ukiachana na upande mpana wa ilmu ya Imam Ali (a.s), ambapo katika ilmu na maarifa yeye ni bahari, na sio kwamba ni bahari tu, bali ni bahari pana katika ilmu. Mazungumzo katika ilmu yake ni marefu sana.
Hata katika vipindi vya Utawala wa Sayyidna Abubakar na Sayyidna Omar, pindi yalipokuwa yakiwajia Maswali magumu, walikuwa wakimuelekeza muulizaji kwamba: Nenda kwa Aba Turab (Ali bin Abi Talib (a.s) ukamuulize, huyo ndiye anaweza kujibu Maswali yako.
Hivyo, sisi kama Waislamu, wafuasi wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), tunasikitika sana kwa kuuliwa Kishahidi Imam wetu na Kiongozi wetu Ali bin Abi Talib (a.s), tena alipigwa upanga wenye sumu kali kichwani mwake akiwa Msikitini anaswalisha Swala ya Alfajiri.
Mwsiho, Samahat Sheikh Said Othman amemalizia nukta kwa kusema kwamba: Huu ni msiba mkubwa mno kwa Umma wa Kiislamu, na sisi Waislamu tunaomboleza na kuhuisha kumbukumbua ya Kifo chake cha Kishahadi (kilichotokea Usiku wa 21 ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan) kwa kufanya Majalisi na Vikao mbalimbali kwa kukumbushana juu ya fadhila na mafunzo mazuri kutoka kwa Kiongozi huyu wa Waumini, Amrul-Muuminina Ali (a.s).
Your Comment