Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA -; Hawzat al_Zahra (s.a) iliyopo chini ya Taasisi ya Bilal Muslim Mission, Tawi la Tanga, katika kuienzi Qur'an Tukufu ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, imefanya hafla ya Mashindano ya Qur'an Tukufu katika vipengele viwili: Kuhifadhi na Kusoma kwa Tartil.
Mudir wa Hawzat Al_Qaim (a.t.f.s), Samahat Sheikh Kadhim Abbas, katika Hafla hiyo ya Mashindano ya kuhifadhi Qur'an aliwakumbusha Waumini umuhimu wa kuisoma na kuienzi Qur'an Tukufu, na akaashiria katika baadhi ya Fadhila za kusoma na kuhifadhi Qur'an Tukufu kama ifuatavyo:
1. Mtu bora kabisa kuliko wengine ni yule anajifunza Qur'an Tukufu na kuifundisha kwa wengine.
2. Yeyote anayeisoma Qur'an Tukufu na anaikariri mara kwa mara huku anaona ugumu mkubwa (katika kutamka, anakwama kwama kwenye utamkaji wake), huyo atapata ujira mara mbili:
3. Watu wote wanaoshikamana na Qur'an Tukufu, hao ni watu bora kabisa Mbele Mwenyezi Mungu (s.w.t).
4. Mfano wa mtu anayeisoma Qur'an, ni kama harufu nzuri na ladha nzuri, kinyume na yule asiyeisoma wala kujali wala kuwa na muda na Qur'an.
5. Yeyote anayeisoma Qur'an Tukufu na kuizingatia, huyo hupata thawabu kwa kila herufi moja atakayoitamka.
6. Yeyote mwenye kuisoma Qur'an Tukufu, basi kwa hakika Qur'an hii itakuwa Muombezi wake Kesho Siku ya Kiyama.
7. Qur'an Tukufu Siku zote humnyanyua mtu hadi katika Daraja za juu, na humdhalilisha asiyeandamana nayo.
8. Yeyote mwenye kuihifadhi Qur'an Tukufu na kuifanyia kazi katika maisha yake, huyo atapandishwa Daraja za juu katika Pepo (Jannat).
9. Wale wanaoisoma na kujifunza Qur'an Tukufu; huteremkiwa na Malaika ambao huja na kuwazunguka na kuwapa utulivu na rahma za Mwenyezi Mungu (s.w.t).
10. Kuhifadhi Qur'an Tukufu na kujifunza na kuzijua maana ya Aya za Qur'an Tukufu, ni bora zaidi kuliko mapambo yote ya Dunia.
11. Mtu mwenye kujishughulisha na kuhifadhi Qur'an Tukufu, atavalishwa Taji Siku ya Kiyama.
12. Muislamu mwenye kuhifadhi Qur'an Tukufu na mwenye Elimu juu ya Qur'an Tukufu, huyo atakuwa ni mwenye kuangaziwa na Nuru ya Qur'an kaburini mwake, na Mtume Muhammad (s.a.w.w) atakuwa Shahidi wake kesho Siku ya Kiyama.
Mashindano haya, yamehudhuriwa na Masheikh wa Hauzat Al_Qaim (a.t.f.s), pamoja na wageni kutoka sehemu mbalimbali za Jiji la Tanga.
Aidha, waliohudhuria ni pamoja na Waumini wa Kike kutoka katika Taasisi kadhaa za Kishia zilizopo katika Jiji la Tanga, halikadhalika Taasisi za Kisunni.
Washindi katika Mashindano haya wamepewa zawadi mbalimbali zenye thamani kutoka katika Taasisi ya Bilal Muslim Mission, Tanga Branch.
Your Comment