27 Machi 2025 - 15:44
Source: Parstoday
Mkuu wa Kikosi cha Quds: Iran itaendelea kuwa bega kwa bega na Palestina kwa operesheni za kijeshi

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko thabiti katika msimamo wake wa kuunga mkono kadhia ya Palestina kupitia uungaji mkono wa moja kwa moja kwa vikosi vya Muqawama na kwa operesheni za kijeshi kama zile za Ahadi ya Kweli.

Jenerali Esmaeil Qa’ani aliyasema hayo jana Jumatano katika kipindi cha "Minbari ya Quds" kilichorushwa hewani kwa njia ya intaneti na kujumuisha hotuba za viongozi kadhaa wa Muqawama kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds itakayoadhimishwa kesho Ijumaa duniani kote.

Qa’ani ameipongeza Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa na harakati ya Hamas Oktoba 7, 2023 akiielezea kuwa ni "mchanganyiko wa Muqawama wa kwenye medani ya vita na Muqawama wa wananchi".

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC amebainisha kuwa,  operesheni hiyo "iliibua dhana mpya ya umoja baina ya mirengo ya Muqawama," na kudhihirisha nguvu na mshikamano wa vikosi vya Muqawama.

Jenerali Esmaeil Qa’ani ametilia mkazo uungaji mkono usioyumba wa Jamhuri ya Kiislamu Iran kwa vuguvugu la mapambano na Muqawama na kusisitiza kwamba, uungaji mkono huo "utaendelea hadi litakapofikiwa lengo kuu la kuikomboa Quds".

Viongozi kadhaa wa Muqawama akiwemo Khalil al-Hayya wa Hamas, Ziad al-Nakhalah wa Jihadul-Islami ya Palestina, Sheikh Naim Qassem wa Hizbullah ya Lebanon na Abdul-Malik al-Houthi wa Ansarullah ya Yemen nao pia walihutubia programu hiyo ya Minbari ya Quds.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha