27 Machi 2025 - 15:46
Source: Parstoday
Trump asaini amri ya kubadilisha mfumo wa uchaguzi na upigaji kura Marekani, apingwa vikali

Rais wa Marekani Donald Trump amesaini amri ya kiutekelezaji ya kubadilisha mfumo wa uchaguzi na upigaji kura wa nchi hiyo, inayojumuisha sharti la uthibitisho wa uraia kwa usajili wa wapiga kura.

Hati ya amri hiyo iliyotolewa kwa anuani ya ‘Kuhifadhi na Kulinda Uadilifu wa Uchaguzi wa Marekani,’ inatoa wito kwa majimbo kutoa ushirikiano kwa mashirika ya serikali ya shirikisho na kuyapatia orodha ya wapigakura, pamoja na kushtakiwa wanaohusika na makosa ya uhalifu wa uchaguzi. Aidha, inatishia kupunguza ufadhili wa kifedha wa serikali kuu kwa majimbo ambayo yatashindwa kutekeleza agizo hilo.

Pamoja na mambo mengine, amri hiyo ya utekelezaji iliyotolewa na Trump inaagiza kuwepo na uthibitisho wa uraia ili wapiga kura waweze kuandikishwa katika chaguzi za shirikisho.

Hata hivyo, mashirika ya kutetea haki ya upigaji kura yamekosoa mabadiliko hayo yanayopendekezwa yakisema, Wamarekani wengi wenye umri wa kupiga kura hawana uthibitisho wa uraia unaoweza kupatikana kwa urahisi. Kulingana na ripoti ya 2023 iliyokusanywa na Kituo cha Haki cha Brennan pamoja na makundi mengine, watu wapatao milioni 21.3, yaani karibu 9% ya raia wa Marekani walio katika umri wa kupiga kura, hawana hati kama hizo.

Chini ya agizo hilo la Trump, ambaye amekuwa kwa muda mrefu akikosoa mfumo wa uchaguzi na upigaji kura wa Marekani ukiwemo wa kupiga kura kwa njia ya posta, sasa ni lazima kura "zipigwe na kupokelewa" kabla ya siku ya uchaguzi, huku ufadhili wa kifedha wa serikali kuu ukishurutishwa na hatua ya majimbo ya kutii agizo hilo.

Hatua hiyo tayari imekabiliwa na ukosoaji wa vyama mbalimbali ambavyo vimeapa kuipinga mahakamani. Waziri wa mambo ya nje wa Jimbo la Oregon, Tobias Read, amesema agizo hilo ni "hatua iliyo dhidi ya demokrasia" kutokana na jimbo hilo kutegemea sana mfumo wa upigaji kura kwa njia ya posta.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha