Mnamo Februari, utawala wa Trump uliliweka genge hilo kwenye orodha ya mashirika ya kigaidi, na sasa inadai kwamba genge hilo liliingia Marekani kwa msaada wa serikali ya Venezuela.
Trump ameandika katika mtandao wa kijamii wa "Truth Social" kwamba: "Venezuela imekuwa na uadui mkubwa na Marekani na uhuru ambao tunauunga mkono." Kwa hivyo, nchi yoyote inayonunua mafuta au gesi ya Venezuela italazimika kulipa ushuru wa asilimia 25 katika biashara yoyote na nchi yetu (Marekani)."
Kwa mujibu wa tangazo hilo, ushuru huu utaanza kutekelezwa Aprili 2, na nchi zilizoathirika zina wakati mchache wa kuzoea hali hiyo.
Kutoza ushuru mkubwa wa kibiashara ni mojawapo ya mbinu ambazo Trump amekuwa akizitimia wakati wa utawala wake ili kutoa mashinikizi dhidi ya nchi tofauti pinzani. Kwa hakika Trump amegeuza matumizi ya ushuru wa juu wa biashara kuwa nguzo kuu ya sera zake za kiuchumi, kijamii na kidiplomasia ili kuwawekea mashinikizo wapinzani wa Washington na kuzifungamanisha nchi mbalimbali na matakwa ya Marekani.
Trump, ambaye anakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi nchini Marekani, anadai kwamba anaweza kuyalazimisha makampuni na viwanda vya nchi hiyo kurejea nchini kwa kuweka ushuru wa juu na usio wa kawaida. Pia anadai kwamba hali hiyo itasaidia kupunguza nakisi ya biashara na bajeti, kuongeza ajira na kuimarisha nafasi ya Marekani katika nyanja za kimataifa na kupanga hali ya kiuchumi.
Kuhusiana na hilo, hivi karibuni alitumia ushuru wa forodha kutoa mashinikizo dhidi ya Colombia ili ikubali kupokea wahamiaji haramu wake walioko Marekani. Canada, Mexico, na Uchina pia zimetishia kulipiza kisasi kwa kuiwekea Marekani ushuru wa juu wa biashara.
Kuhusu Venezuela, kwa upande mmoja Trump anafuatilia ushindi wa kibiashara wa Marekani, na kwa upande mwingine, bado anajaribu kutoa mashinikizo dhidi ya Venezuela ili kumuondoa madarakani rais halali wa nchi hiyo, Nicolás Maduro, na kuweka mahala pake serikali tegemezi itakayohudumia maslahi ya Washington.
Kwa hakika, watawala wa Marekani hawastahimili kuona upinzani wa miaka mingi wa Maduro wa kutotekeleza matakwa ya Marekani pamoja na siasa zake za kibeberu na ukoloni, hivyo wamekuwa wakitumia njia na mbinu mbalimbali kwa ajili ya kuwashinikiza raia wa Venezuela na kutaka kumpindua Maduro. Kuhusiana na hili, tunaweza kutaja matumizi ya siasa za vikwazo vya kiuchumi, hasa katika sekta ya fedha, benki na nishati, pamoja na uungwaji mkono wa vyama vya upinzani dhidi ya Maduro katika miaka kumi iliyopita kama mfano wa wazi wa mbinu hizo. Hata hivyo, siasa hizi zimeshindwa kufikia lengo lake hadi hadi sasa ambapo Maduro ameweza kudhibiti migogoro na kurekebisha hali ya mambo nchini kwa ushirikiano wa wananchi. Kuhusiana na hilo, Maduro amesema mara kwa mara kuwa nchi yake itaendelea kujitawala na kupinga ubeberu wa kigeni na kusisitiza kuwa watu wa Venezuela kamwe hawatakuwa watumwa wa mtu yeyote.
Pia amesema mtu au kampuni yoyote iliyo tayari kuwekeza nchini Venezuela itakaribishwa kufanya hivyo ndani ya mfumo wa sheria za nchi hiyo na makubaliano yenye manufaa kwa pande zote mbili.
Ni wazi kuwa Trump ameanza duru mpya ya utawala wake kwa kutoa mashinikizo dhidi ya Venezuela. Mapema mwezi huu, alitoa makataa ya siku 30 kwa ajili ya kubatilishwa leseni iliyotolewa mwaka 2022 na ambayo iliruhusu kampuni ya mafuta ya Chevron ya Marekani kuendesha shughuli zake huko Venezuela na kuuza nje mafuta yake.
Kwa hakika, kwa kuweka ushuru mpya wa mafuta na gesi, mbali na kuilenga moja kwa moja Venezuela na uchumi wake, Trump pia amewalenga washindani wa Marekani, haswa China. China huagiza mapipa milioni 240 ya mafuta ghafi kutoka Venezuela kila siku, na ushuru huo mpya bila shaka utaathiri uchumi wa China pia.
Licha ya siasa na mashinikizo yote hayo ya Marekani, lakini viongozi wa Venezuela kwa mara nyingine tena wamesisitiza kuwa wataendelea kutetea na kulinda kujitawala kwa nchi hiyo kwa nguvu zao zote. Akizungumzia kujitawala huko mkabala wa uingiliaji wa kigeni, Maduro amesema: "Hapa, amani, kazi na umoja wa kitaifa vitashinda tu."
342/
Your Comment