Kulingana na ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA -, waandamanaji wasiopungua 19 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa huko Abuja siku ya Ijumaa.
Picha za video za matukio hayo zinaonyesha vikosi vya jeshi la Nigeria vikilinda eneo hilo huku waandamanaji wakikimbia kujificha na huku milio ya risasi ikisikika. Picha hizo pia zinaonyesha askari wakiburuta maiti ya raia mtaani na kuitupa kwenye gari huku wakiwapiga waandamanaji wengine wawili na kuwalazimisha kuingia kwenye lori jingine.
Tume ya Kiislamu ya Haki za Kibinadamu (IHRC) imelezea wasiwasi wake juu ya mashambulizi dhidi ya waandamanaji baada ya kufichuliwa kuwa mamlaka ya Nigeria walikuwa wakifanya maandalizi katika suala hili kama kisingizio cha shambulio hilo.
Ofisi ya Mshauri wa Usalama wa Taifa ilisisitiza ulazima wa kusitisha maandamano ya Siku ya al-Quds ili "kuzuia uvunjifu wa amani" unaofanywa na waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina, hii ni kwa mujibu wa barua ya ndani iliyovuja na iliyoonekana na IHRC.
Katika taarifa hiyo iliyovuja, viongozi wa Nigeria walikuwa wameonya kwamba ingawa maandamano ya wafuasi na waungaji mkono wa Palestina yalikuwa ya amani, waandamanaji kuna uwezekano wakaamua kutafuta / kudai haki kwa kushambulia maslahi ya Marekani na Israel nchini humo. Kwa hiyo, maandamano yao lazima yasimamishwe.
Mbinu hii imekuwa ikitumiwa na maafisa wa Nigeria wanaoiunga mkono Israel katika miaka ya hivi karibuni ili kuvifanya vikosi hivyo kufanya msako mkali dhidi ya waandamanaji.
Ikumbukwe kuwa: Takriban mtu mmoja aliuawa, na wengine wengi kujeruhiwa baada ya Polisi kufyatua risasi kwenye maandamano ya Siku ya Quds huko Abuja mnamo 2023.
Mnamo 2014, vikosi vya usalama vya Nigeria viliwaua waandamanaji 34 baada ya kufyatua risasi kwenye mkutano huko Zaria.
Maandamano ya kila mwaka ya Siku ya Quds Duniani kote hufanywa na waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina katika Ijumaa ya Mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu (na wasiokuwa Waislamu) ili kuonyesha mshikamano wao na Wananchi Madhulumu wa Palestina.
Your Comment