30 Machi 2025 - 17:29
Source: Parstoday
Azma ya Iran ya kutekeleza operesheni ya tatu ya kijeshi dhidi ya Israel

Mshauri mwandamizi wa kijeshi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amethibitisha kwamba Iran itatekeleza operesheni ya tatu ya kijeshi dhidi ya utawala wa Israel katika kujibu vitendo vya uchokozi vya utawala huo dhidi ya Iran.

Akizungumza Ijumaa, Meja Jenerali Yahya Rahim Safavi amesema"Ikiwa Operesheni ya Ahadi ya Kweli III haijatekelezwa bado, kuna hekima katika kuchelewesha, si kwamba imefutwa."

Amesema kuchelewesha huko ni hatua ya kimkakati na kutokana na hekima ya makusudi.

Afisa huyo amesema Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni wenye "hekima, ujasiri, mwenye maono ya mbele, na wa busara," huku akibaini kwamba operesheni hiyo itatekelezwa kwa wakati muafaka kwa uamuzi wa Ayatullah Khamenei.

Tamko hilo limekuja chini ya wiki moja baada ya Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran Meja Jenerali  Mohammad Bagheri kusisitiza kwamba Iran imeendeleza “vipimo vyote vya kujihami vinavyohitajika kwa ajili ya kuwa na uwezo wa  kijeshi ambao ni mara kumi zaidi ya ule uliotumika wakati wa Operesheni Ahadi ya Kweli II."

Mwaka jana, Jamhuri ya Kiislamu ilionyesha nguvu zake za kijeshi katika Operesheni za Ahadi ya Kweli I na II, ambapo ilitekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi kufuatia uchokozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Operesheni hizo, zilizoendeshwa kwa kutumia mamia ya makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani au droni, zilionyesha uwezo wa Iran wa kushambulia malengo nyeti ya kijeshi na kijasusi ya Israeli kwa usahihi.

Maafisa wa Iran wamesisitiza kwamba jeshi lilitumia sehemu ndogo tu ya nguvu zake za kivita wakati wa operesheni hizo mbili za kulipiza kisasi.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha