30 Machi 2025 - 17:30
Source: Parstoday
Iran yalaani shambulio la anga la Israel dhidi ya Beirut

Iran imelaani vikali shambulio kubwa la anga la utawala haramu Israel kwenye maeneo ya makazi katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yalifikiwa kati ya utawala huo na harakati ya Muqawama ya Lebanon, Hizbullah.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema Ijumaa kwamba shambulio hilo lilitokea katika Siku ya Kimataifa ya Quds wakati kukiwa na kauli ya kimataifa ya kuchukizwa na uvamizi wa utawala wa Israel na mauaji ya kimbari huko Palestina.

Ameongeza kuwa hatua ya "kijambazi" ya utawala ghasibu wa Israel ilikiuka waziwazi mipaka ya Lebanon.

Baghaei amesema kwamba Umoja wa Mataifa na wasimamizi wa makubaliano ya kusitisha mapigano wana jukumu la moja kwa moja kuhusiana na shambulio hilo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za haraka na madhubuti kukabiliana na vitendo vya ukatili vya utawala wa Israel na kuzuia uvunjaji wake wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Israel ilifanya shambulio katika vitongoji vya kusini vya Beirut Ijumaa, ikiwa ni  shambulio kubwa la kwanza tangu makubaliano ya kusitisha mapigano kumaliza vita kati ya utawala wa uvamizi na Hizbullah mnamo Novemba.

Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Lebanon, Jeanine Hennis-Plasschaert, amesema ufyatulianaji risasi mipakani kati ya Lebanon na utawala wa Israel Ijumaa ni jambo ambalo limeibua "wasiwasi mkubwa."

Pia Ijumaa, Israel ilifanya mashambulizi ya kikatili katika Lebanon ya kusini.

Baada ya kuhimili hasara kubwa katika miezi 14 ya mzozo na kutofanikiwa katika malengo yake katika operesheni dhidi ya Lebanon, Israel haikuwa na budi ila kukubali kusitisha mapigano na Hezbollah. Makubaliano ya kusitisha mapigano yalianza kutekelezwa  mnamo Novemba 27.

Tangu yaanza kutekelezwa, vikosi vya utawala haramu wa Israel vimekuwa vikifanya mashambulizi dhidi ya Lebanon, vikivunja makubaliano ya kusitisha mapigano, ambayo yanajumuisha mashambulizi ya anga katika taifa hilo la Kiarabu.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha