Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA -; Sheikh Izzud - Din wa Kenya, baada ya kudai kuzuiwa kutoa Mawaidha Zanzibar, na kulituhumu Baraza la Ulamaa la Zanzibar kuwa kuna baadhi ya watu ndani yake si watu wazuri katika utendaji wao, amerudi na kuwaomba samahani watu kadhaa kadhaa aliowataja na kuwagusia katika ufafanuzi wake wa awali akisema: " Niliongea na kutawaliwa na hisia zangu na "emotional" yangu, hilo likapelekea nikaongea kwa kukosea na ikawa ni kukosoa kosa kwa kufanya kosa".
Baada ya kukaa na kufikiri na kutafakari, nimeona kuwa nimeruhusu hisia zangu zinitawale na kunisukuma kusema niliyoyasema. Na mimi ni Mwanadamu nimekosea, na sikufurahia kukosea kwangu. Nakiri kosa langu kwa sababu nimekosea Kibinadamu.
Hivyo leo tarehe 30, 03, 2025, nimeamua kutoka hadharani katika Mitandao yote kuomba radhi kutoka na kile nilichokisema na nikakosea kusema, kwa sababu nilitumia njia mbaya kusema, na sikutakiwa kusema nilivyosema.
Hivyo, natumia fursa hii kumuomba radhi Rais wa Tanzania, Dr.Samia Suluhu Hassan kwa kumhusisha katika mazungumzo yangu.
Na pia, namuomba radhi Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dr. Hussein Mwinyi, kwa sababu nilihusisha pia katika maongezi yangu.
Pia, namuomba radhi Sheikh wangu, Mufti Mkuu wa Zanzibar.
Pia, namuomba radhi Rais wangu wa Kenya, Dr.Samuel Ruto, kwa kumtaja katika maongezi yangu, sikuwataja wote kwa dharau au kutokuwaheshimu, bali haikuwa na haja kuwataja katika Mazungumzo yangu.
Pia, nawaomba radhi Wapenzi wangu kwa kuwashirikisha pia katika maongezi yangu, na kuwafanya wawe na hisia mbaya na Mufti wa Zanzibar au Ofisi ya Mufti.
Binafsi nina furaha kuwa Mwenyezi Mungu amenipatia fursa ya kuomba msamaha nikiwa bado niko hai, natamani ningesimama hata juu ya Al_Kaaba Tukufu nikaomba msamaha hadharani. Kwa hakika, sihisi udhalili kuomba msamaha hadharani, bali ningejihisi udhalili kwa kujiona niko sahihi na sijakosea lolote.
Nawausia wengine, tuwe makini katika kuongea, na tusiongee kwa kufuata hisia zetu, na tuwe makini na maneno yetu tunaponena, kuna wataalamu wa kuchambua maneno tunayonena.
Your Comment