Alkhamisi iliyopita ya tarehe 3 Aprili, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, likarefusha muda wa kuhudumu Ripota Maalumu wa baraza hilo wa masuala ya Iran na kupiga kura ya kuongeza muda usio na kikomo wa shughuli za Kamati ya Kutafuta Ukweli kuhusu Iran. Azimio hilo lilipitishwa katika kikao cha 58 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika mjini Geneva kwa kura 24 za ‘ndiyo’, 8 za ‘hapana’ na nchi 15 hazikupiga kura.
Azimio hilo limekosolewa vikali na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ukosoaji wa Iran umejumuisha nukta zifuatazo:
Kwanza ni kwamba, azimio hilo lilipendekezwa na Uingereza na Marekani, nchi mbili ambazo daima zimekuwa na sera na mtazamo wa chuki na uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa hivyo kimsingi, lengo hasa la waandaaji wa azimio hilo ni kulitumia kisiasa na kutoa mashinikizo kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na vitisho vya serikali ya Donald Trump dhidi ya Tehran. Kuhusiana na suala hilo, Ali Bahreini, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amewakosoa waandaaji wa Ulaya wa azimio hilo na kusema: “waandaaji wa rasimu ya azimio wanajaribu kulipotosha Baraza hili kwa kujenga taswira potofu ya hali ya haki za binadamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran”.
Pili ni kuwa, azimio hili limepitishwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hali ambayo jinai zisizo na kifani na ambazo hazijawahi kushuhudiwa zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ghaza zingali zinaendelea, lakini Baraza la Haki za Binadamu na wanachama wake wa Ulaya hawajachukua hatua yoyote kuhusiana na jinai hizo. Wakati huo huo nchi kama Ujerumani na Ufaransa ambazo zilichangia pendekezo la azimio hilo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimo kwenye kundi la waungaji mkono na washirika wa utawala wa Kizayuni katika mauaji ya kimbari ya watu wa Ghaza. Esmail Baghai Hamaneh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria hatua zilizochukuliwa na Uingereza, Ujerumani, Canada, na waandaaji na waungaji mkono wengine wa azimio dhidi ya Iran katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kuhusiana na majanga mbalimbali ya haki za binadamu yaliyojiri katika eneo la Magharibi mwa Asia, hususan mauaji ya kimbari ya Ghaza na jinai nyingine za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Lebanon na Syria, na akasema: “si Uingereza, -ambayo yenyewe ni mmoja wa waungaji mkono wakubwa zaidi wa kisiasa, kifedha na wa silaha wa utawala wa Kizayuni, huku waziri wake wa mambo ya nje akidai kuwa inahitaji mamilioni ya watu wauawe ili kuthibitisha kuwa kinachotokea Ghaza ni mauaji ya kimbari- wala si Ujerumani, -ambayo ni msambazaji wa pili mkubwa wa silaha zilizotumiwa na Israel katika mauaji ya kimbari na ambayo waziri wake wa mambo ya nje ametamka kinagaubaga kuwa mauaji ya watoto na wanawake wasio na hatia wa Kipalestina yanakubalika-, zina ustahiki wowote wa kimaadili wa kuwapa somo watu wengine kuhusu haki za binadamu."
Lakini tatu ni kwamba, kutawala siasa badala ya sheria katika utendaji kazi wa Baraza la Haki za Binadamu ambalo ni taasisi ya kisheria, linakifanya chombo hicho cha Umoja wa Mataifa kipoteze heshima na itibari yake mbele ya serikali na macho ya walimwengu; na wakati huo huo, kupoteza itibari kunafungua njia ya kupoteza ufanisi wake pia, kama ulivyopoteza itibari pia Umoja wa Mataifa katika kipindi hiki cha miaka miwili kutokana na maafa ya Ghaza na Lebanon. Ali Bahreini, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amekosoa vikali taratibu za ufuatiliaji za kibaguzi na kiupendeleo zilizotumika katika azimio dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba, hatua hiyo italitumbukiza Baraza la Haki za Binadamu kwenye kinamasi kipya cha utendaji mbovu na wa ufujaji wa rasilimali na kupelekea kupungua itibari ya taasisi hiyo.
Ukweli wa mambo ni kuwa Iran ni nchi yenye historia na ustaarabu mkubwa ambayo daima imekuwa ikijivunia mafanikio yake yaliyoifaidisha jamii ya wanadamu na imechukua hatua muhimu za kulinda haki za binadamu na uhuru wa kimsingi wa wananchi wake kwa mujibu wa Katiba na sheria zilizowekwa pamoja na hati na mikataba ya kimataifa iliyopasishwa na serikali ya Iran. Azimio la Baraza la Haki za Binadamu dhidi ya Iran, zaidi ya kitu chochote kile ni hatua ya ulaghai na udanganyifu na ya kutumiwa vibaya kisiasa baraza hilo na baadhi ya nchi…/
342/
Your Comment