7 Aprili 2025 - 22:59
Source: Parstoday
Meja Jenerali Bagheri: Majibu ya Iran kwa barua ya Marekani yametolewa kwa msingi wa mantiki na nguvu

Mkuu wa Majeshi ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si mpenda vita, lakinii itakabiliana vikali kitendo chochote cha uonevu na uchokozi.

Meja Jenerali Mohammad Bagheri amesisitiza stratijia ya Iran ya kutetea maslahi ya taifa na kuelekea kwenye malengo yaliyoainishwa, akiashiria operesheni za kijeshi zilizopewa jina la "Ahadi ya Kweli", ambako Iran ilijaribu uwezo wa nguvu na udhaifu wa maadui zake. Amesema: "Katika makabiliano ya kijeshi na utawala wa Kizayuni wa Israel na utekelezaji wa Operesheni Ahadi ya Ukweli, tulijaribu ipasavyo uwezo, nguvu na udhaifu wa adui na sisi wenyewe, na tuliweza, katika muda mfupi sana, kutatua kwa usahihi baadhi ya mambo. Sasa, na kwa taarifa sahihi nasema kwamba, hali ya ulinzi wetu wa anga, kiwango cha uzalishaji na uwezo wa makombora na ndege zetu zisizo na rubani ni cha juu zaidi na hakiwezi kulinganishwa na wakati wa operesheni Ahadi ya Kweli."

Meja Jenerali Bagheri amelaani kimya cha kutisha na undumakuwili wa taasisi za kimataifa eti za kutetea haki za binadamu kuhusiana na jinai na ukatili wa utawala wa Kizayuni katika mauaji ya kimbari ya watu wasio na hatia, watoto, wanawake na vikongwe huko Gaza na kusema: Uovu, mauaji ya kimbari ya watu wasio na hatia na uharibifu wa makazi ya watu huko Gaza na Lebanon unaofanywa na utawala wa Kizayuni baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa unafanyika kwa himaya na msaada wa utawala wa Marekani, nchi za Ulaya na katika kivuli cha undumakuwili na kimya cha aibu cha taasisi za kimataifa eti za kutetea haki za binadamu. 

Mkuu wa Majeshi ya Iran amemtaja rais mpya wa Marekani kuwa ni mbabe na mchokozi na kusema: "Leo hii dunia inashuhudia kwamba anazozana hata na marafiki na washirika wake, sambamba na maadui zake."

Akiashia yaliyomo katika majibu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa barua ya Rais Donald Trump wa Marekani, Meja Jenerali Mohammad Bagheri amesema, Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa Iran haitaanzisha vita lakini itajibu vitisho vya aina yoyote kwa nguvu zote. Na kuhusu suala la nyuklia, hatutafuti kuunda silaha za nyuklia, na hatutafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani, lakini hakuna ubaya na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja. Amesema barua hiyo imemtaja Trump kuwa ndiye mtu mbaya zaidi wa kukengeuka makubaliano na kwa msingi huo Iran haina imani naye.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha