7 Aprili 2025 - 23:06
Source: Parstoday
Araghchi: Hakujakuwa na mazungumzo yoyote kati ya Iran na Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesisitiza tena kuwa Iran iko tayari kufanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani, lakini amebainisha kuwa hadi sasa hakuna duru yoyote ya mazungumzo ya moja kwa moja iliyowahi kufanyika kati ya mataifa hayo mawili.

Akizungumza pembezoni mwa kikao na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni siku ya Jumapili, Araghchi alifafanua hali ya hivi karibuni ya mazungumzo yanayohusiana na Iran na Marekani.

Amesema: “Hadi sasa, hakuna duru yoyote ya mazungumzo baina ya Iran na Marekani iliyofanyika.”

Araghchi amebaini kuwa Iran imeshatangaza msimamo wake kuwa iko wazi kwa diplomasia na mazungumzo, japo kwa njia zisizo za moja kwa moja.

Hata hivyo, kauli za Marekani zimekuwa zikitofautiana. Rais wa Marekani ameitaka Tehran kuingia kwenye mazungumzo ya moja kwa moja kuhusu mpango wake wa nyuklia, huku akitishia kuivamia kijeshi iwapo diplomasia itashindwa.

Mnamo Machi 30, Rais wa Marekani, Donald Trump, alitishia kuishambulia Iran na kuiwekea vikwazo vya ziada iwapo Tehran haitafikia makubaliano na Washington juu ya mpango wake wa nyuklia. Alipozungumza na NBC News, Trump alidai kuwa maafisa wa Iran na Marekani wana mawasiliano, ingawa hakutoa maelezo ya kina.

Iran kwa upande wake imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba haitaketi kwenye meza ya mazungumzo na serikali ya Marekani hadi pale Washington itakapositisha kampeni yake ya vitisho na mashinikizo.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, siku ya Jumamosi alikosoa vikali lugha ya vitisho dhidi ya Tehran, akisema kuwa taifa lake liko tayari kwa mazungumzo “kwa usawa.”

Pezeshkian alisema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatafuta mazungumzo kwa msingi wa usawa. Wanaitishia Iran kwa mkono mmoja, kisha wanataka kuzungumza kwa mkono mwingine.”

Naye Mkuu wa Majeshi ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si mpenda vita, lakinii itakabiliana vikali kitendo chochote cha uonevu na uchokozi.

Meja Jenerali Mohammad Bagheri amesisitiza stratijia ya Iran ya kutetea maslahi ya taifa na kuelekea kwenye malengo yaliyoainishwa, akiashiria operesheni za kijeshi zilizopewa jina la "Ahadi ya Kweli", ambako Iran ilijaribu uwezo wa nguvu na udhaifu wa maadui zake.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha