10 Aprili 2025 - 19:49
Source: Parstoday
Araqchi: Uhusiano wa Iran na Algeria uko imara, ni wa kihistoria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Algeria ni nchi kubwa na yenye taathira katika Ulimwengu wa Kiislamu na kwamba uhusiano kati ya nchi hiyo na Iran ni mkubwa, imara na wa siku nyingi.

Sayyid Abbas Araqchi amesema baada ya kutembelea Msikiti Mkuu wa Algeria kwamba: "Mwishoni mwa ziara yangu, niliweza kutembelea Msikiti Mkuu wa Algeria. Msikiti ambao ni nembo ya Muqawama, mapambano ya ukombozi na Jihadi ya taifa la Algeria dhidi ya ukoloni, na ni nembo ya kushikamana kwao na imani za kidini, maadili na utambulisho wao wa Kiislamu."

Araqchi amekumbusha kuwa uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Algeria ni mkubwa, imara na wa siku nyingi na kuongeza kuwa: Nchi mbili  zina msimamo wa pamoja na unaoshabihiana kuhusu masuala muhimu ya Ulimwengu wa Kiislamu, hasa kuhusu kadhia ya Palestina. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa uhusiano wa kihistoria umeanzishwa kati ya mataifa ya Iran na Algeria na Mungu akipenda, ushirikiano huu utadumishwa katika siku zijazo. 

Mkuu wa chombo cha diplomasia wa Iran ameitaja Algeria kuwa ni nchi kubwa na yenyy taathira katika Ulimwengu wa Kiislamu na kusema: Algeria ambayo sasa ni mwanachama katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ina nafasi muhimu na ya juu na inatambulika kama mwakilishi stahiki wa Waislamu na nchi za Kiislamu katika taasisi hiyo ya kimataifa. 

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha