Hayo yamo kwenye taarifa ya jana ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ambayo pia imesema kuwa, ili kupunguza hali ya wasiwasi katika eneo la Asia Magharibi na kuzuia kutokea mgogoro mkubwa zaidi, kuna wajibu wa kuongezwa juhudi za kidiplomasia za kuilazimisha Israel ikomeshe jinai zake huko Ghaza.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya mazungumzo ya simu kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Misri ambapo Tehran imeonesha wasiwasi wake mkubwa kutokana na uwezekano wa kuzuka mvutano wa pande zote wa kikanda kutokana na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ghaza, Lebanon na Syria, pamoja na mashambulizi ya anga ya Marekani nchini Yemen.
Katika mazungumzo yake ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Misri, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa mwito wa kuchukuliwa hatua za pamoja za kikanda ili kuilazimisha Israel iache kuwashambulia wananchi wa Ghaza na kusisitiza kwamba, ufunguo wa utatuzi wa migogoro yote ya eneo hili ni kukomeshwa jinai na uchokozi wa utawala wa Kizayuni katika ukanda huu.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty amesisitizia haja ya kulindwa usalama wa usafiri wa baharini kwenye Bahari Nyekundu na kuhimiza pande zote kuwa wavumilivu na kutoruhusu hali tete iliyopo igeuke kuwa mvutano mkubwa wa kikanda na kimataifa.
Mashambulizi ya Marekani nchini Yemen yanasababisha hasara za kiuchumi kwa nchi nyingi ikiwemo Misri, kiasi kwamba mwezi uliopita wa Machi, Misri ilisema kuwa, kila mwezi inapoteza takriban dola milioni 800 kutokana na hali ya wasiwasi iliyotokea kwenye Bahari Nyekundu kwa sababu ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya Yemen na ulipizaji kisasi wa jeshi la Yemen dhidi ya meli za Marekani na vyombo vya usafiri vya Israel.
342/
Your Comment