11 Aprili 2025 - 18:36
Source: Parstoday
Kimya cha dunia mkabala wa jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa Gaza imekuwa machinjioni, na zaidi ya mwezi mmoja sasa hakuna msaada wowote uliopelekwa eneo hilo na kwamba wakazi wa Gaza hawana mafuta, dawa na bidhaa nyingine zinazohitajika.

Ni wazi kuwa, kwa kukatwa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Gaza, hali ya hofu imeibuka tena, na Gaza imekuwa uwanja wa mauaji na wakazi wake wanaandamwa na kivuli cha mauti usiku na mchana.  

Antonio Guterres ametoa tahadhari hiyo katika hali ambayo msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO) pia ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuendelea kuzuia misaada ya kitiba kuingizwa katika Ukanda wa Gaza, na ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo kukabiliana na maafa ya binadamu katika eneo hilo. 

Ripoti zinaeleza kuwa, Israel imefunga njia zote za kuingiza misaada ya kibinadamu Ukanda wa Gaza; na wakazi wa eneo hilo hawana akiba yoyote ya chakula wala dawa. Viongozi wa Israel wanadai kuwa misaada iliyopelekwa Gaza iko mikononi mwa Hamas. Wakati huo huo, Israel yenyewe imepiga marufuku kuingizwa bidhaa za chakula na misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na inalitumia suala hilo kama silaha dhidi ya Wapalestina wanaoishi katika eneo hilo. Ni dhahir shahir kuwa utawala wa Kizayuni umezuia huduma zote za chakula, dawa na vifaa tiba na hata maji ya kunywa kwa ajili ya Wapalestina ikiwa ni katika kuendeleza sera zake za mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. Kuhusu suala hili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema: Israel ambayo ni dola ghasibu, inawajibu mahsusi mkabala wa sheria za kimataifa ikiwa ni pamoja na sheria za kimataifa za masuala ya kibinadamu. 

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, utawala wowote vamizi una jukumu la kudhamini chakula na dawa za matibabu, na kuhakikisha ulinzi wa taasisi, huduma za matibabu, hospitali na afya ya umma. Hata hivyo licha ya kanuni zote hizi za kisheria, si tu kuwa hakuna misaada ya kibinadamu inayoruhusiwa kuingia Gaza bali Israel inawashambulia pia wafanyakazi wa taasisi za kimataifa za misaada ya kibinadamu. 

Kimya cha dunia mkabala wa jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza

Israel inauwa hata wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu 

Sera za kutenda jinai za Israel dhidi ya Wapalestina kama vile mashambulizi ya kikatili yasiyo na ukomo, kukata huduma ya maji na umeme, kuzuia misaada ya kitiba na bidhaa za chakula na kuzuia kuhamishwa majeruhi wa vita, yote haya yanadhihirisha nia ya utawala huo ya kutaka kuwapigisha magoti Wapalestina; Sera ambayo waangalizi wengi wa kimataifa wameitaja kuwa ni jinai ya kivita" au hata "maangamizi ya kizazi." Pamoja na haya, Israel inaendeleza mshambulizi ya kinyama bila kujali sheria na matakwa ya kimataifa ikisaidiwa kikamilifu na Marekani na waitifaki wake wengine. Waungaji mkono wa Israel pia wanaendelea kuipatia Israel silaha, msaada wa kiintelijinsia na kuuhami kisiasa na kimataifa ili kuzuia mashinikizo ya kisheria kwa utawala huo.

Ni wazi kuwa, Israel kama wanavyokiri weledi wengi wa mambo, imefeli katika vita dhidi ya Gaza na sasa imejikita katika kutekeleza sera za maangamizi ya kizazi na kuwalazimisha Wapalestina kuhama nchi na ardhi yao ya asili. 

Wakati huo huo, maandamano yanaendelea kushuhudiwa katika pembe mbalimbali duniani dhidi ya jinai za Israel. Huko Misri maelfu ya raia wa nchi hiyo wameandamana sambamba na safari ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika mji wa bandari wa Arish katika Jangwa la Sinai. Maandamano hayo yamefanyika kulaani sera ya kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina na njama za Wazayuni za kutaka kuwahamishia Wapalestina katika Jangwa la Sinai. Wananchi wa Morocco pia wamefanya maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Rabat na kusisitiza uungaji mkono wao madhubuti na wa wazi kwa Muqawama na Palestina. Aidha wamelaani vita vya mauaji ya kimbari, sera za kuwatesa kwa njaa Wapalestina na kuzuia misaada kuingia Gaza kunakofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina. 

Kimya cha dunia mkabala wa jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza

Maandamano ya Wamisri mkabala wa ziara ya Macron huko Arish 

Waandamanaji katika miji ya Brussels, London, Paris, Istanbul, Seoul, Amman na katika nchi nyingine nyingi wanaopinga sera za uvamizi wa Israel, wamelaani mashamulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina.

Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International pia limetangaza katika ripoti yake kwamba Israel imefanya mauaji makubwa na kuwasababishia Wapalestina hali mbaya ya maisha kwa kukusudia kuangamiza sehemu ya jamii ya Wapalestina. 

Licha ya jamii ya kimataifa kutaka kukomeshwa jinai za utawala wa Kizayuni katika ukanda wa Gaza lakini kuendelea uungaji mkono na misaada ya Marekani kwa Israel, sambamba na kimya cha baadhi ya nchi za Magharibi na Kiarabu, kivitendo kunafutilia mbali uwezekano wa kusitishwa hali ya mgogoro, na hii ni sawa na kushirikiana na watenda jinai hao wa Kizayuni.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha