Akizungumza katika mkutano wa siku mbili huko Pantin, viungani mwa Paris, Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa UN kuhusu Palestina ameashiria ukiukaji wa mara kwa mara wa utawala wa Israel wa usitishaji vita ulioanzishwa mwezi Januari na kusisitiza kwamba, bila ya uingiliaji kati wa jamii ya kimataifa, jinai za kivita za Israel zitaendelea kuwepo.
"Israel haitasitisha hatua zake," Albanese amesema, akisisitiza kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anatumia vita vya Gaza kukwepa kubebeshwa dhima ya ukiukaji wake wa sheria za kimataifa.
"Nadhani sina matumaini tena katika mfumo wa haki wa Israel au ngazi ya kimataifa, kwa sababu unaona kila mtu akisema yuko tayari kumtandikia (Netanyahu) zulia jekundu," amesema. Ameeleza kuwa, mataifa kadhaa ya Magharibi na Ulaya yamempokea Netanyahu, na kupuuza kabisa hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ametoa indhari kuhusu hali ya janga la kibinadamu inayozidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya umoja huo mjini New York, Guterres amesema “zaidi ya mwezi mzima umepita bila ya hata tone moja la msaada kufika Gaza”. Amefafanua kwa kusema: “hakuna chakula. Hakuna mafuta. Hakuna dawa. Hakuna bidhaa za kibiashara.”
342/
Your Comment