Kamandi Kuu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imethibitisha tena nguvu isiyotetereka na uimara wa hali ya juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika kulinda ardhi na watu wa Iran.
Katika taarifa ya Jumapili iliyotolewa kuadhimisha miaka 46 tangu kuanzishwa kwa IRGC, Kamandi Kuu ya Majeshi amesisitiza pia kuhusu moyo wa kujitolea, ujasiri, na uwezo wa kikosi hicho kukabiliana na tishio lolote bila kujali ukubwa au nguvu za adui.
Taarifa hiyo imeashiria jukumu la IRGC katika kukabiliana na vitisho vya ndani na vya nje, hasa kupitia mapambano dhidi ya makundi ya kihalifu, magaidi wakufurishaji, na mahasimu wa kiserikali kama vile Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israeli.
Taarifa hiyo ilieleza mafanikio ya operesheni kama Ahadi ya Kweli I na Ahadi ya Kweli II mwaka 2024, ambapo IRGC ilitekeleza mashambulizi ya mafanikio dhidi ya malengo nyeti na ya kimkakati ya Israel kwa kutumia makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani, kama hatua ya kujibu uchokozi wa Tel Aviv dhidi ya ardhi ya Iran.
Aidha, taarifa hiyo ilikumbusha kuwa kikosi cha IRGC kilianzishwa na Imam Khomeini, aliyeongoza Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 yaliyomuondoa mfalme wa kiimla, Shah, aliyekuwa kibaraka wa Marekani, na kisha kuasisi Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa hivyo, Jeshi la IRGC ni zao la moyo wa Mapinduzi, na limekabidhiwa jukumu la kulinda malengo na misingi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, kwa kufuata miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, IRGC imeendelea kuimarisha uwezo wa ulinzi na wa kuzuia mashambulizi dhidi ya taifa, na kuhakikisha usalama wa taifa na watu wake.
Zaidi ya ulinzi, juhudi za IRGC zimeenea kwenye maeneo ya ustawi wa jamii, maendeleo ya kiuchumi, na kujitegemea kwa taifa.
IRGC pia imehusika katika masuala mengine nyeti kama vile ujenzi na kupunguza umaskini, na imetajwa kuwa na mchango mkubwa katika miradi mikubwa ya miundombinu.
Kamandi ya Majeshi ya Iran imeelezea matumaini kuwa IRGC pamoja na vikosi vingine vya ulinzi vya Iran vitaendelea kusimama imara mstari wa mbele katika kulinda Mapinduzi ya Kiislamu.
342/
Your Comment