Siku ya Jumamosi, mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, yakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi na Steve Witkoff, mwakilishi maalumu wa Rais wa Marekani katika Mashariki ya Kati, yalifanyika nchini Italia kwa uratibu wa Oman.
Kwa mujibu wa Pars Today, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi amesema katika mahojiano aliyofanyiwa jana na Shirika la Habari la Tasnim: "kwa matazamo wetu, maudhui ya mazungumzo hayo ni ya nyuklia, na sisi tunafungamana na suala hili; na ni wazi kwamba, kwa uoni wetu, suala jengine lolote ghairi ya kuaminisha kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni wa amani ili mkabala wake viondolewe vikwazo, si maudhui ya mazungumzo".
Kuhusiana na hilo Araghchi amesema: "hadi sasa, wao (Wamarekani) wamezingatia suala hili".
Kuhusu matokeo ya mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "tulikuwa na mazungumzo ya muda wa masaa manne. Katika muendelezo wa mazungumzo yaliyopita, mara hii pia tumepiga hatua mbele. Tumefanikiwa kufikia maelewano mazuri zaidi kuhusiana na baadhi ya misingi na malengo kadhaa. Imepangwa kuwa mazungumzo yaendelee na kuingia katika awamu zinazofuata, na kuanza vikao vya wataalamu".
Aliongezea kwa kusema: "mazungumzo ya kiufundi katika ngazi ya wataalamu yatafanyika Oman kuanzia Jumatano ya wiki hii. Jumamosi ijayo tutakutana tena nchini Oman na kuhakiki matokeo ya kazi ya wataalamu".
Araghchi amebainisha kuwa, mazungumzo ya Rome yalifanyika katika anga ya kujenga na kwa kupiga hatua mbele.
Kuhusiana na uvumi unaoenezwa kuhusu mazungumzo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "dhana na tafsiri binafsi zenye malengo tofauti huwepo kila mara katika mazungumzo yoyote yale. Sithibitishi yoyote kati ya dhana hizo. Wakati yazungumzo yatakapofikia kwenye mwafaka, ndipo yatakapoonyesha natija yake".../
342/
Your Comment