21 Aprili 2025 - 23:03
Source: Parstoday
Papa Francis afariki dunia akiwa na umri wa miaka 88

Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88, katika makazi yake ya Casa Santa Marta, ndani ya jiji la Vatikan.

Kifo cha Papa kilitokea siku moja baada ya kuonekana kwa muda mfupi mbele ya maelfu ya waumini waliokusanyika katika Uwanja wa Vatikan kwa ajili ya sikukuu ya Jumapili ya Pasaka.

Hotuba yake ya Pasaka ilisomwa na msaidizi wake huku yeye akiwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu, akiitazama. Baadaye, alizungushwa kwa gari katika uwanja huo wa Vatikan.

Papa Francis alilazwa katika Hospitali ya Agostino Gemelli Polyclinic siku ya Ijumaa, tarehe 14 Februari 2025, baada ya kuugua kwa siku kadhaa kutokana na bronkaitisi.

Hali ya kiafya ya Papa Francis iliendelea kudhoofika, na madaktari wake waligundua kuwa alikuwa na nimonia ya pande zote mbili (bilateral pneumonia) siku ya Jumanne, tarehe 18 Februari.

Baada ya siku 38 hospitalini, Papa marehemu alirudi katika makazi yake ya Casa Santa Marta kuendelea na mapumziko ya afya.

Jorge Mario Bergoglio, ambaye baadaye alichukua jina la Papa Francis, alichaguliwa kuwa papa mnamo Machi 13, 2013, jambo lililowashangaza wengi waliokuwa wakifuatilia siasa za Kanisa, kwani padri huyo kutoka Argentina alionekana kuwa mtu wa nje ya mfumo wa kawaida.

Papa Francis alirithi Kanisa lililokuwa katika mgogoro mkubwa kutokana na kashfa ya unyanyasaji wa kingono wa watoto, pamoja na migogoro ya ndani ya utawala wa Vatikan, na alichaguliwa akiwa na dhamira ya kurejesha nidhamu na utulivu.

Hata hivyo, kadri kipindi chake cha uongozi kilivyokuwa kikiendelea, alikumbwa na upinzani mkali kutoka kwa wahafidhina waliomtuhumu kwa kuvunja mila za jadi za Kanisa. Vilevile, alikosolewa na wanamabadiliko waliodhani hakuenda mbali vya kutosha katika kulibadilisha Kanisa hilo lenye historia ndefu.

Papa Francis aliteua karibu asilimia 80 ya makadinali wapiga kura watakaomchagua Papa ajaye, jambo linaloongeza uwezekano kwamba mrithi wake ataendeleza sera zake za kimabadiliko, licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa wahafidhina.

Wakati huo huo, Munther Isaac, mchungaji na mwanateolojia mashuhuri Mkristo wa Kipalestina, ameeleza pole zake kufuatia kifo cha Papa Francis.

Isaac amesema kwamba Papa Francis “alionyesha huruma ya kweli kwa Wapalestina, hasa kwa wale walioko Gaza wakati wa mauaji haya ya kimbari yanayoendelezwa na utawala haramu wa Israel. Ameashiria matamshi makali ya Papa akilaani Israel kwa mauaji yake ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha