Pars Today imeinukuu IRNA na kuripoti kuwa duru ya tatu ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, iliyoanza mapema leo Jumamosi Aprili 26, ilimalizika wakati wa jioni kwa saa za Oman.
Duru hiyo ya tatu ya mazungumzo, kama mbili zilizotangulia iliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi na Mwakilishi Maalumu wa Rais wa Marekani katika Mashariki ya Kati Steve Witkoff kwa uratibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Badr bin Hamad Al Busaidi.
Kwa mujibu wa tangazo la chombo kikuu cha kidiplomasia cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, duru hiyo ya tatu ya mazungumzo imejumuisha pia majadiliano ya kitaalamu na kiufundi, ambapo kwa upande wa Iran timu ya wataalamu iliongozwa na Majid Takht Ravanchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa masuala ya kisiasa na Kazem Gharibabadi, anayehusika na masuala ya kisheria na kimataifa. Michael Anton ndiye aliyeongoza timu ya wataalamu wa Marekani. Anton alikuwa msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa wakati wa muhula wa kwanza wa urais wa Donald Trump.
Imeelezwa kwamba katika mazungumzo ya leo zimepigwa hatua kadhaa muhimu katika kushughulikia masuala ya msingi yanayohusu mpango wa nyuklia wa Iran na suala la kuondolewa vikwazo na imeafikiwa kwamba duru ya nne ya mazungumzo hayo itafanyika tarehe 3 ya mwezi ujao wa Mei.
Duru ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani ilifanyika Jumamosi iliyopita (Aprili 20) huko Roma, mji mkuu wa Italia. Baada ya kumalizika kwa duru hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi aliwaambia waandishi wa habari: "mara hii pia kikao kilikuwa kizuri na ninaweza kusema tumepiga hatua mbele. Mara hii tumefanikiwa kufikia maelewano mazuri zaidi kuhusiana na baadhi ya misingi na malengo kadhaa. Imepangwa kuwa mazungumzo yaendelee na kuingia katika awamu zinazofuata, na kuanza vikao vya wataalamu".../
342/
Your Comment