26 Aprili 2025 - 22:49
Source: Parstoday
Mripuko mkubwa watikisa bandari ya Shahidi Rajaee kusini mwa Iran, 5 wafariki, zaidi ya 500 wajeruhiwa

Mripuko mkubwa umetokea katika bandari ya Shahidi Rajaee kusini mwa Iran na kusababisha uharibifu mkubwa na hasara, huku timu za utoaji huduma za dharura zikikimbilia katika eneo la tukio ili kudhibiti hali hiyo.

Kwa mujibu wa Idara ya kushughulikia matukio ya majanga mkoani Hormozgan, watu wanne wamethibitishwa kufariki dunia hadi sasa na 561 wamejeruhiwa baada ya lori la mafuta kuripuka kwa sababu zisizojulikana katika bandari ya Shahidi Rajaee mapema leo.

Majeruhi wamehamishiwa katika hospitali za Hormozgan.Mkurugenzi Mkuu wa idara ya usimamizi wa matukio ya majanga wa Hormozgan amesema mripuko huo ulikuwa mkubwa sana, lakini chanzo chake hasa bado hakijajulikana.

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa mripuko huo ulianzia katika jengo la utawala ndani ya eneo la bandari. Mripuko huo ulikuwa mkubwa kiasi kwamba ulibomoa kikamilifu jengo hilo na kuharibu pia magari mengi.

Babak Mahmoudi, Mkuu wa Shirika la Misaada na Uokoaji la Iran, amethibitisha kuwa mripuko mkubwa katika bandari ya Shahidi Rajaee umesababisha vifo vya watu wanne, na kuongeza kuwa majeruhi wote 516 wamehamishwa.

"Hadi sasa, watu 516 wamejeruhiwa, na wameondolewa kwenye eneo la tukio. Baadhi yao wamejeruhiwa kwa kuangukiwa na vioo vilivyovunjika na wengi wao walikuwa na majeraha madogo madogo hivyo wameruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu, na hadi sasa watu wanne wamethibitishwa kufariki kwa sababu katika eneo hili kulikuwa na vifaa vya kuhifadhi mada za kemikali," ameeleza Mahmoudi katika mahojiano na televisheni ya Press TV wakati akitoa maelezo ya mripuko huo.

Kwa mujibu wa afisa huyo, mripuko huo ulitokea saa sita kasoro dakika tano mchana kwa saa za huko, na akaongeza kuwa timu kadhaa za utoaji misaada na uokoaji zimetumwa haraka kwenye eneo la tukio na kwamba kuna matumaini ya kudhibitiwa moto huo baada ya saa chache zijazo.

Kufuatia tukio hilo, shughuli zote za bandari zimesitishwa huku vikosi vya usalama na dharura vikifanya kazi ya kulinda eneo hilo. Mamlaka zimetangaza mara moja hali ya dharura katika hospitali zote za mji wa Bandar Abbas ili kujiweka tayari endapo kiwango cha maafa kitakuwa kikubwa.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha